• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:05 PM
Wazo la mawaziri wawe wabunge lashika kasi

Wazo la mawaziri wawe wabunge lashika kasi

CHARLES WANYORO na VITALIS KIMUTAI

MBUNGE wa Chama cha Jubilee ameunga mkono wazo kwamba mawaziri wawe wakichaguliwa kutoka miongoni mwa wabunge ili kuongeza uwajibikaji serikalini.

Mbunge wa Imenti Kusini, Bw Kathuri Murungi alisema kutokana na kuwa wabunge huchaguliwa na wananchi, hawatahitajika kulipwa mishahara mara mbili na watakuwa wakilipwa tu marupurupu ya majukumu.

Anataka wazo hilo ambalo limekuwa likitajwa na viongozi wengi wa kisiasa liwe sehemu ya maswali yatakayojumuishwa kwenye kura ya maamuzi inayopendekezwa.

“Mbunge akiwa waziri hatahitaji kulipwa mishahara mara mbili bali atapata tu marupurupu. Mawaziri 22 hupokea mishahara mikubwa na marupurupu mbali na gharama za wasaidizi wao na magari lakini mbunge hatahitaji hayo yote,” akasema.

Akizungumza wakati wa mkutano wa viongozi kujadili uundaji wa wilaya mpya katika afisi ya naibu kamishna anayesimamia eneo la Imenti Kusini katika soko la Kaguru, Bw Murungi pia alipendekeza nafasi zaidi katika serikali ziundwe ili jamii tofauti ziwakilishwe uongozini.

Aliunga mkono pia uundaji wa wadhifa rasmi wa kiongozi wa upinzani ili mgombeaji urais anayeibuka katika nafasi ya pili, aingie bungeni moja kwa moja na aruhusiwe kuunda baraza la mwigo la mawaziri ambalo litakuwa likilipwa mishahara.

“Endapo utaunda muungano wa kisiasa kabla uchaguzi, inafaa uwe na watu ambao wanawakilisha jamii zote. Ukiteua naibu rais, waziri mkuu, manaibu wawili wa mawaziri, maspika wa bunge la taifa na seneti, manaibu wao na viongozi wa wengi wawe wa kutoka jamii tofauti hiyo itaonyesha sura ya kitaifa,” akasema.

Wandani wa Naibu Rais William Ruto wamekuwa wakipinga uundaji wa nafasi zaidi katika serikali kuu kufaidi wanaoshindwa uchaguzini.

Wakiongozwa na Seneta wa Kericho, Bw Haron Cheruiyot na Mbunge wa Kikuyu, Bw Kimani Ichung’wa, wabunge walio wandani wa Bw Ruto walitoa wito kwa Wakenya kujihadhari na wanasiasa ambao wanataka kuteka kura ya maamuzi kwa manufaa yao ya kibinafsi.

“Sote tunafahamu vyema kwamba kuna viongozi wanaotaka kutumia kura ya maamuzi iliyopendekezwa kubuni nafasi zitakazofaidi wanaoshindwa uchaguzini katika serikali kuu,” akadai Bw Cheruiyot.

Aliongeza, “Hatupingi kura ya maamuzi, ileteni lakini mjue hata mkijaribu kubadilisha katiba ili kubuni nafasi kusaidia wanaoshindwa uchaguzini, rais ajaye wa nchi hii atakuwa Dkt Ruto.”

Wabunge hao walikuwa wakizungumza katika kijiji cha Kaproret mnamo Jumapili wakati wa hafla ya kutoa shukrani iliyoandaliwa na Mbunge Mwakilishi wa Kaunti ya Kericho, Bi Florence Koech ambayo ilihudhuriwa na Naibu Rais.

“Hatuogopi kura ya maamuzi kama inavyodaiwa na baadhi ya watu. Tunaomba wanaotaka kura ya maamuzi walete maswali yao ili tuyajadili. Tutaunga mkono kura hiyo kama italeta umoja kwa wananchi na kubuni nafasi za ajira kwa Wakenya,” akasema Bw Ichung’wa.

Aliongeza kuwa Wakenya wanahitaji kutilia maanani zaidi utekelezaji wa ajenda nne kuu za maendeleo kwani zitaboresha uchumi na kuwezesha uwekezaji zaidi.

  • Tags

You can share this post!

Simu ya Uhuru ilitumika kwa ulaghai wa Sh10 milioni,...

‘Sijuti kamwe kukataa nyumba ya bure kutoka kwa...

adminleo