Habari Mseto

Wenye hoteli na waraibu wa pombe waendelea 'kupimiwa hewa'

July 29th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMMY WAWERU

SERIKALI imesisitiza kuwa haitalegeza masharti ya kupinga pombe kuuzwa katika hoteli na vituo vya kupika vyakula vinavyouzwa na kubebwa vikiwa tayari.

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe amesema marufuku hayo yanalenga kuzuia mkusanyiko wa watu ili kudhibiti kuenea kwa Covid-19.

Akitoa onyo kali kwa wamiliki wa mikahawa na hoteli, Bw Kagwe alisema Jumanne serikali haitasita kuadhibu watakaokiuka masharti.

Aidha, waziri alisema leseni za wahusika kuhudumu zitapigwa marufuku kabisa.

“Mtu akitaka kula nyama, si lazima nyama iandamane na pombe. Hata soda ni sawa, inaenda sambamba na nyama,” akasema.

“Kama unauza kitu yoyote ile ya kula, usiuze pombe. Kama ulianza kuuza mandazi na samosa ili uuze pombe, sahau pombe. Uza hayo mandazi na samosa pekee,” waziri akaeleza mnamo Jumanne, wakati akihutubia wanahabari Afya House katika kikao cha kutoa taarifa ya maambukizi ya corona nchini, muda wa saa 24 zilizopita.

Kagwe alisema “huu ni wakati wa waraibu wa pombe kurejea nyumbani wakiwa soba.”

“Huwa unaona mtu na macho mekundu kila siku asubuhi na jioni, saa hii tunataka kuwaona wakiwa na macho meupe. Tunataka kuona watu wakienda nyumbani mapema na wakiwa soba,” Kagwe akaeleza, akisema marufuku ya mvinyo kuuzwa katika hoteli inasaidia kuzuia watu kukiuka sheria na mikakati iliyowekwa kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona.

Kauli ya Bw Kagwe ilijiri siku moja baada ya Rais Uhuru Kenyatta kupiga marufuku vileo kuuzwa katika hoteli. Rais pia alisisitiza kwamba mabaa yangali yamefungwa, hadi notisi itakapotolewa.

Akitilia mkazo amri ya Rais, Waziri Kagwe amewataka wamiliki wa mabaa kuiheshimu.

“Kama uko na baa yako, usiifungue, usifungiwe. Ukifungiwa, utaanza kuenda kuchunga ng’ombe ilhali hujui. Ukifungiwa shauri yako, fuata yale masharti serikali inasema,” akasema, akisisitiza kwamba watakaokiuka amri hiyo serikali haitakuwa na budi ila kufutilia mbali kabisa leseni zao.

Kwa waraibu wa pombe, waziri Kagwe alisema wasiibuke na mpango B na C, kuinunua na kuinywea nyumbani kwa kuandaa hafla zitakazohatarisha maisha ya watu wa familia hasa watoto na wakongwe.