Wenye majengo jijini wapewa siku 14 kuyapaka rangi lau sivyo yafungwe
KAUNTI ya Nairobi imetangaza makataa ya siku 14 kwa wamiliki wa majengo, wapangaji na maajenti kusafisha na kupaka rangi upya majengo yao au waadhibiwe vikali ikiwemo kushtakiwa na majengo kufungwa.
Kulingana na agizo hilo lililotiwa saini na Kaimu Katibu wa Kaunti, Godfrey Akumali, majengo yote katikati mwa Jiji Kuu pamoja na mitaa ya Westlands, Upper Hill, Ngara, Kirinyaga Road na vituo vyote vya kibiashara, lazima yatimize viwango vya afya ya umma na makazi.
Akumali alisema agizo hilo linafuata Sheria ya Afya ya Umma (Sura 242) na Sheria ya Mipango ya Ardhi na Matumizi ya Ardhi ya mwaka 2019, likilenga kuboresha mwonekano wa jiji na kulinda afya ya umma.
Amri hiyo inaanza kutumika mara moja kwa muda wa siku 14 pekee. Wanaokaidi watafungiwa majengo na kushtakiwa chini ya vifungu vya 115, 118 na 126 vya Sheria ya Afya ya Umma.
Gavana Johnson Sakaja ameondoa ada za vibali vya kupaka rangi kipindi hiki, kufuatia hoja ya Bunge la Kaunti iliyolenga kurembesha sura ya jiji.
MCA wa Kilimani, Moses Ogeto, alisema Nairobi ni uso wa taifa na makao ya mashirika ya Umoja wa Mataifa kwa hivyo inapaswa kuwa na mwonekano mzuri.
Wakazi sasa wanasubiri kuona kama Gavana Sakaja atatekeleza agizo hilo kikamilifu.