• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 2:19 PM
Westgate: Korti kuhukumu wawili

Westgate: Korti kuhukumu wawili

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA Jumatano iliwapata washukiwa wawili – waliozuiliwa kuhusiana na shambulio la jengo la kibiashara la Westgate Mall lililosababisha vifo vya watu 67 – kuwa na hatia.

Hakimu Mkuu, Bw Francis Andayi, aliwapata wawili hao kuwa na hatia, baada ya kuzuiliwa kwa miaka saba, tangu waliposhtakiwa kwa kushirikiana na magaidi wa Al Shabaab katika shambulio hilo.

Kufuatia uamuzi huo, Bw Andayi aliamuru Mabw Mohamed Ahmed Abdi na Hussein Hassan Mustafa, wazuiliwe hadi Oktoba 22, 2020, atakapowahukumu baada ya kupokea ripoti ya wahasiriwa wa shambulio hilo.

Akiwasilisha ombi la wahasiriwa wahojiwe ndipo maoni yao yazingatiwe kabla hukumu kupitishwa, kiongozi wa mashtaka, Bw Edwin Okello, alisema, “maelfu ya watu walijeruhiwa, biashara kuharibiwa, watu kuathiriwa kimawazo na familia za walioangamia wanahitaji kutoa maoni kuhusu athari za tukio hilo.”

Bw Okello alieleza mahakama kwamba sheria siku hizi inatoa mwanya kwa wahasiriwa kuchangia kabla ya hukumu kupitishwa dhidi ya washtakiwa.

“Naomba hii mahakama ipatie afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), siku 14 kuwahoji wahasiriwa wa shambulizi hilo kisha iwasilishe ripoti hiyo kortini kabla ya hukumu kupitishwa,” Bw Okello aliomba.

Pia mawakili Victoria Wanjiku na Mwihaki Gikonyo wanaomwakilisha Bw Mohamed Ahmed Abdi na Bw Chacha Mwita anayemwakilisha Bw Hussein Hassan Mustafa, waliomba ripoti ya afisa wa urekebishaji tabia na kitengo cha kupambana na visa vya kigaidi wawahoji washtakiwa hao pia na ripoti kuwasilishwa.

Mahakama ilikubali ombi hilo la Bw Okello na Bi Wanjiku na Bi Gikonyo na “kuamuru ripoti hizo ziwasilishwe kortini Oktoba 22 ndipo mawakili wawasilishe tetesi za mwisho dhidi ya washtakiwa.”

Mahakama iliwataka mawakili waandae tetesi za washtakiwa kabla hukumu kupitishwa.

Mahakama inaweza kutoa kifungo cha maisha dhidi ya washtakiwa.

Wakati huo huo, mahakama ilimwachilia huru mshtakiwa wa tatu, Bw Liban Abdullahi Omar, ikisema kuwa ijapokuwa simu yake ilipigwa mara 79, haiwezi kuamuliwa kuwa alikuwa anawasiliana na waliotekeleza shambulio kwa vile ilipigwa na ndugu yake Ahmed Hassan Abubakar, ambaye alikuwa mmoja wa washambuliaji hao.

“Hii mahakama ilitilia shaka kwamba simu yake iliyokuwa inapigwa na nduguye marehemu ilikuwa inapanga njama hizo,” alisema Bw Andayi.

Hakimu alisema washumbulizi hao walikuwa wanawasiliana na washtakiwa hao hadi walipofika katika eneo la kuegesha magari katika jengo hilo la Westgate.

  • Tags

You can share this post!

Vijana wahamasishwe badala ya kutumiwa vibaya – mbunge

Giroud ashikilia nafasi ya pili katika orodha ya wafungaji...