Weta kukabili wimbi la ‘Tawe’ la Natembeya
JOTO la kisiasa linatokota Magharibi mwa Kenya huku mvutano wa ubabe ukionekana kuchipuka baina ya Spika wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetang’ula na Gavana wa Kaunti ya TransNzoia, George Natembeya.
Gavana Natembeya aliyeinuka uongozini kufuatia umaarufu wake kama Kamishna mchapakazi naye Spika Wetangula anajivunia tajriba ya miaka mingi kama mwanasiasa tangu 1992 na waziri, huku mgogoro baina yao ukimburura Waziri wa Afya, Susan Nakhumicha katikati.
Rais William Ruto, Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi na kiongozi wa chama cha Democratic Action Party-Kenya (DAP-K) Eugene Wamalwa, wanaotoka Trans Nzoia pia wamejumuishwa kwenye vuta ni kuvute hiyo.
Bw Natembeya, anayeongoza Vuguvugu la Tawe (Imetosha) anamwona Spika wa Bunge la Kitaifa kama kizingiti cha maendeleo eneo hilo na tishio kwa azma yake kuchaguliwa tena kama gavana.
Bw Wetang’ula hajaficha nia yake ya kuwa kigogo wa Magharibi.
Bi Nakhumicha aliwania kiti cha Mwakilishi Mwanamke Trans Nzoia kwa tiketi ya Ford Kenya katika Uchaguzi Mkuu 2022 na kuibuka wa tatu akiwa na kura 32, 497 ambapo mgombea wa UDA Lilian Chebet Siyoi, aliibuka mshindi akifuatiwa na Phanice Khatundi wa DAP-K aliyepata kura 65,641.
Duru zinasema huenda anamezea mate ugavana 2027 akiungwa mkono na kiongozi wa Ford Kenya.
Kwa upande wake, Bw Mudavadi anashinikiza ANC ivunjiliwe mbali ili ajiunge na UDA ya Rais Ruto, uamuzi utakaozidisha shinikizo kwa Ford Kenya ya Wetang’ula, ambayo imesisitiza haitavunjiliwa mbali.
Haya yamejiri huku Bw Wamalwa, anayeegemea Muungano wa Raila Odinga wa Azimio la Umoja, akisubiri kujinufaisha kutokana na utengano huo na kutumia chama chake cha DAP-K, ambacho Bw Natembeya ni mwanachama wake, kupata uungwaji mkono katika eneo hilo lenye idadi kubwa ya watu.
Huku akikabiliwa na shinikizo la kuvunja chama chake pamoja na upinzani mkali kutoka kwa Bw Natembeya, Ford Kenya imesema inaunda mpango wa kuzima tishio hizo na kwamba wataibuka wakiwa imara zaidi.
Katibu Mkuu wa Ford Kenya John Chikati amesisitiza bosi wake hana kinyongo na Gavana akisema Ford Kenya ina umaarufu mkubwa Trans Nzoia.
“Trans Nzoia si nyanja ya kigeni kwa Wetang’ula wala Ford Kenya. Chama cheti kimekuwapo kwenye kiti cha ugavana hapo awali. Sasa, ushindani unashika kasi kwa sababu ya udhibiti, lakini tupo tayari kukabiliana nao ana kwa ana. Tutajitahidi kuvutia watu kujiunga na Ford Kenya, yote bila kusita kutukana wala kujibizana,” alisema Bw Chikati.
Kuhusu uwezekano wa kutengwa na Kenya kwanza, alizungumzia uhusiano wa Ford Kenya na vyama vinginevyo katika kambi hiyo akitaja mtazamo mmoja kama msingi wa ushirikiano wao.