Habari MsetoSiasa

Wetang'ula atisha kutoboa siri zote za Raila Odinga

May 29th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na PATRICK LANG’AT

KIONGOZI wa Ford-Kenya Moses Wetang’ula ametisha kuanika hadharani siri za kiongozi wa ODM Raila Odinga iwapo ataendelea kuwachokoza.

Hii ni baada ya kinara huyo wa ODM kudai kuwa mpango wa kutaka kuunganisha vyama vya Ford Kenya na ANC chake Musalia Mudavadi ni wa kikabila.

Mnamo Jumapili Bw Odinga alipuuzilia mbali hatua ya Bw Mudavadi na Bw Wetang’ula kutaka kuunganisha vyama vyao kwa lengo la kuleta pamoja jamii ya Waluhya.

Bw Odinga alisema mpango huo unalenga kugawanya Wakenya kwa misingi ya kikabila.

Lakini, jana, Bw Wetang’ula alisema kuwa Bw Odinga anahofia kuwa muungano wa vyama vya ANC na Ford-Kenya utasambaratisha azma yake ya kutaka kuwa rais 2022.

“Tunamtaka Bw Odinga kukoma kutuchokoza. Asiturushie mawe ilhali anaishi kwenye nyumba ya vioo. Akiendelea kueneza madai ya uongo kutuhusu, tutafichua siri zake kwa kueleza ukweli kumhusu,” akasema Bw Wetang’ula.

Mabwana Odinga, Bw Mudavadi na Wetang’ula na Bw Kalonzo Musyoka wa Wiper walikuwa vinara wenza wa muungano wa National Super Alliance (Nasa) uliobuniwa Januari 2017 kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi wa Agosti 8, mwaka jana.

Lakini muungano huo ulisambaratika baada ya Bw Odinga kuafikiana kufanya kazi na Rais Uhuru Kenyatta mnamo Machi 9, mwaka huu.

Bw Wetang’ula pia alipokonywa wadhifa wake wa Kiongozi wa Wachache katika Seneti.

“Raila anapoungwa mkono na jamii ya Waluo si ukabila, lakini jamii nyingine zinapounga mkono viongozi wao anawaita wakabila. Huku ni kujikanganya.

Nilisema kuwa talaka yetu itakuwa yenye kelele na vurugu na sasa Raila ameanza kuhisi joto,” Bw Wetang’ula akaambia Taifa Leo afisini kwake jijini Nairobi.

“Raila amegundua kwamba amepoteza uungwaji mkono katika eneo la Magharibi. Wafuasi wamemkimbia. Naona akiwania urais tena 2022 lakini tutakutana kwa debe,” akaongezea.

Bw Wetang’ula alisema kuwa muungano wa vyama vya Ford-Kenya na ANC huenda ukajumuisha chama cha Wiper.

Vyama vya ANC na Ford Kenya tayari vimebuni jopo la watu 10 linaloongozwa na Dkt Boni Khalwale na Katibu Mkuu wa ANC Barrack Muluka kuandaa mikakati ya kubuni chama kipya.