Habari Mseto

Wetang'ula: Lengo letu ni kuwaunganisha Wakenya

March 14th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na CECIL ODONGO
VIONGOZI mbalimbali wameunga mkono juhudi za kuunganisha taifa hili haswa baada ya mkutano wa Ijumaa iliyopita kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa NASA Raila Odinga.
Akizungumza Jumatano kwenye misa ya kumuaga msomi marehemu Prof Oeri Tumbo katika kanisa la Consolata Shrine Mtaani Westlands, Kiongozi wa wachache kwenye Bunge la seneti Moses Wetang’ula alisema kwamba wanalenga kuunganisha taifa na kuleta maridhiano.
Kiongozi huyo aliyefikisha rambirambi za vinara wenzake alimsifu marehemu kama msomi aliyeshirikiana nao kupigania mfumo wa vyama vingi mapema miaka ya 90.
“Prof akishirikiana na wengine kama Marehemu Job Omino na Ooko ombaka walitufaa kwa mawaidha ya kuikomboa nchi kutoka kwa uongozi wa chama kimoja,” akasema Wetangu’la.
Kwa upande wake, Seneta wa Kisii Prof Sam Ongeri alisema kwamba amani ni kiungo muhimu nchi inapokua na kusifia mwelekeo ambao nchi imechukua tangu mkutano kati ya viongozi hao wakuu.
Akimwomboleza marehemu Prof.Ongeri alisema kwamba jamii ya Abagusii wamempoteza shujaa aliyetumia ujuzi alionao kuwasaidia bila kubagua .
“Alikuwa msomi,mwanafamilia na mchanganuzi wa maswala ibuka katika jamii na tunashukuru Mungu kwa maisha yake hapa duniani,” akaongeza Seneta huyo.
Misa hiyo pia ilihudhuriwa na Jaji Mkuu David Maraga na Wasomi kutoka Vyuo Vikuu mbalimbali nchini na nje na wanafamilia akiwemo Mbunge wa Kitutu Chache Kusini Richard Onyonka ambaye ni mpwa wa mwendazake.
Marehemu ambaye kwa wakati moja alikuwa Mkuu wa Kitengo cha Sayansi ya Bayolojia Chuo cha Chiromo bewa la Chuo Kikuu cha Nairobi alitambuliwa mno kutokana na kushiriki mijadala ya kuchanganua maswala yanayoathiri taifa kwenye Vyombo vya habari haswa runinga.
Atazikwa Ijumaa nyumbani kwake katika Kaunti ya Kisii, eneobunge la Kitutu Chache Kusini.