Habari Mseto

Wezi wavamia nyumba ya daktari wa Cuba, waiba na kula chakula chake

September 19th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na George Odiwuor

POLISI mjini Homa Bay wanachunguza kisa ambapo watu wasiojulikana walivunja nyumba ya daktari wa Cuba, wakaiba vifaa vya kielektroniki na kula chakula chake.

Wezi hao waliingia nyumbani kwa Bi Blanco Torres, ambaye ni daktari wa masuala ya familia katika Kaunti ya Homa Bay, Jumatano saa tisa asubuhi wakaiba televisheni, redio, kifaa cha kusaga chakula, na jiko la kupasha chakula moto.

Washukiwa walikuwa na hata muda wa kupasha moto chakula kilichokuwa ndani ya friji ya Dkt Torres, na kula kwa starehe.

Wakati huu wote, Dkt Torres alikuwa amejifungia ndani ya chumba cha kulala akisikiza yote yaliyokuwa yakiendelea.

“Nilikuwa nimetoka tu kuzungumza kwa simu na familia yangu nchini Cuba nikawa najitayarisha kwenda kitandani niliposikia mtu akitembea ndani ya nyumba yangu. Nikaamua kuwa kimya nisimshtue aliyekuwa ndani ya nyumba,” alisema akieleza kuhofia kupiga mayowe asije akashambuliwa.

Maafisa wawili wa polisi waliokuwa wakilinda nyumba ya daktari huyo pia watachunguzwa.