• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 6:46 PM
Wiper yamuonya Ruto kujisifia ushindi Embakasi

Wiper yamuonya Ruto kujisifia ushindi Embakasi

Na CHARLES WASONGA

CHAMA cha Wiper kimeonya mrengo wa Naibu Rais William Ruto katika Jubilee, dhidi ya kudai ndio uliochangia ushindi wa mgombeaji wake katika uchaguzi mdogo wa Embakasi Kusini.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, Katibu Mkuu wa chama hicho Judith Sijenyi, alisema chama hicho kimechukizwa na madai ya wafuasi wa Dkt Ruto kuwa ndio waliowezesha ushindi wa Bw Julius Mawathe.

“Tunawaonya baadhi ya wanasiasa wakome kutukera kwa kujaribu kuvuna mahala ambako hawakupanda,” Akasema Bi Sijenyi.

Ingawa taarifa yenyewe haikutaja chama cha Jubilee, inaaminika kuwa Wiper ilikuwa ikimjibu Dkt Ruto na wandani wake, ambao walichangamkia ushindi wa Bw Mawathe (Embakasi Kusini) na David Ochieng’ (Ugenya) wakidai ni ishara ya ushindi kwao.

Dkt Ruto aliandika ujumbe wa pongezi kwa wawili hao akisema ushindi wao ulionyesha wananchi wa kawaida wameamua kufanya maamuzi kivyao bila kuingiliwa.

Nao maseneta Kipchumba Murkomen (Elgeyo Marakwet), Aaron Cheruiyot (Kericho) na wabunge Ndindi Nyoro (Kiharu), Didmus Barasa (Kimilili), Oscar Sudi (Kapseret) wakijitokeza waziwazi kudai kuwa ushindi wa Bw Ochieng’ na Bw Mawathe ulikuwa ni ushindi kwa Dkt Ruto.

Walidai kuwa ushindi wa wawili hao ni ishara ya mambo yatakavyokuwa katika kinyang’anyiro cha urais 2022, ambapo walibashiri kuwa Dkt Ruto atamwangusha Bw Odinga.

Mnamo Januari, wabunge wa Jubilee, Charles Njagua (Starehe), George Theuri (Embakasi Magharibi), Benjamin Gathiru (Embakasi Central), Simon Mbugua (Bunge la Afrika Mashariki), na Moses Kuria (Gatundu Kusini) walikutana na Bw Mawathe na kutangaza kumuunga mkono. Hii ilikuwa baada ya Jubilee kutangaza kujiondoa katika kinyang’anyiro hicho na kuunga mkono mgombeaji wa ODM.

“Ushindi wa wagombeaji wetu Mheshimiwa Ochieng’ na Mheshimiwa Mawathe ni kionjo tu cha hali itakavyokuwa 2022. Watu wa Ugenya walijitokeza kwa wingi baada ya kuambiwa kuwa kura kwa Ochieng’ ni kura kwa Ruto,” akasema Bw Nyoro.

Wanasiasa wanaomuunga mkono Dkt Ruto wamekuwa wakijibizana vikali na wenzao wa upande wa Bw Odinga kuhusiana na siasa za 2022.

  • Tags

You can share this post!

Mshangao watoto wa miaka 9 na 6 kufunga ndoa

Sonko awaokoa walioshindwa kulipa bili za hospitali

adminleo