• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
Wito afisi ya kijinsia ifufuliwe Baringo

Wito afisi ya kijinsia ifufuliwe Baringo

NA GEOFFREY ONDIEKI

Mwakilishi Mwanamke wa Kaunti ya Baringo Gladwell Cheruiyot ametoa wito kwa Inspekta mkuu wa polisi Hilary Mutyambai kufufua afisi ya kijinsia kwa kila kituo cha polisi ili kusaidia kupunguza visa vya dhuluma za kijinsia nchini.

Mwakilishi huyo alikiri kuwa ofisi ya kijinsia ni muhimu katika vita dhidi ya dhuluma za kijinsia pamoja na visa vya ubakaji.

“Wanawake wanahitaji uangalifu maalum wakati wa kuripoti visa vinavyohusiana na dhuluma za kijinsia, ndio maana tunataka ofisi hiyo ya kijinsia ifufuliwe kwa kila kituo cha polisi,” alisema Bi Cheruiyot.

Aidha Mbunge huyo alisema kuwa wanawake na watoto hupitia wakati mgumu wanaporipoti visa vinavyohusiana na dhuluma za kijinsia na ubakaji, kwa sababu ya ukosefu wa maafisa wa polisi wenye ujuzi kukabiliana nao.

Aliongeza kuwa kuripoti visa vya dhuluma za kijinsia kwenye makao makuu ya polisi huwa kizuizi kwa wahasiriwa kufichua yale wanayoyapitia.

“Ni vigumu kwa wahasiriwa kuripoti masuala nyeti waziwazi. Wakati mwingine wanapozungumza kwenye vituo vikuu vya polisi, hukosa ujasiri wa kujieleza vilivyo,” alisema.

Kiongozi huyo alipendekeza kuwa ofisi hiyo itengewe jumba maalum mbali na vyumba vikuu vya polisi, mbali na kuwa na vyumba vya kibinafsi ndani yake ili kuhudumia wanawake na watoto.

Kulingana na Bi Cheruiyot, maafisa ambao wanafanya kazi katika ofisi hizo za kijinsia wananafaa kuunganishwa na wafanyikazi wa sekta ya huduma za afya ili kuleta ufanisi. Alisema hili litasaidia kuhudumia manusra wa visa kama ubakaji kwa wakati.

“Tunaomba mkuu wa polisi afufue vituo hivi na viwe vinatoa huduma masaa ishirini na manne ili kupunguza visa vya dhuluma ya kijinsia,” alisema Bi Cheruiyot.

Kulingana na kiongozi huyo, wakati mwingine wanawake wanaogopa kuripoti visa vya dhuluma za kijinsia kwa kuogopa watawala kama vile polisi.

“Kuna haja ya kuwapa mafunzo wanapolisi wetu ili wawe na huruma na utu wakati wa kushughulikia masula ya dhuluma za kijinsia,” alisema.

Aliongeza kuwa wanawake wengi wanaodhulumiwa hukimbilia polisi kama chaguo la mwisho wakati wamekosa usaidizi.Kulingana naye hili linatokana na sifa mbaya ya wanapolisi wanaposhughulikia maswala ya kijinsia.

Aliwahimiza wahasiriwa wa dhuluma za kijinsia kukoma kusuluhisha visa hivyo kinyumbani na badala yake kuripoti ili haki itendeke.

You can share this post!

Uchafuzi wa mito huanza kwenye chemchemi

Harambee Starlets kuvaana na Ethiopia kirafiki

adminleo