Habari Mseto

Wito EACC ipige msasa ugavi ardhi

September 12th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na ANTHONY KITIMO

WAKAZI wa Kwale wameitaka Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), kuchukua hatua ya haraka na kuchunguza ugawaji wa ardhi kwa watu mashuhuri kando ya barabara ya pembeni ya Dongo Kundu na kuwaacha wakazi bila makao.

Mamia ya wakazi wamelalamika kuwa Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC), imevuruga orodha ya watu ambao walipaswa kulipwa fidia na kuwapa watu kutoka sehemu nyingine ploti kando ya barabara hiyo ambayo itaunganisha kaunti za Mombasa na Kwale.

“Tunataka asasi husika kuchunguza jinsi maafisa wa serikali na wafanyabiashara walipata ploti katika ardhi yetu huku sisi wenyeji tukiambulia patupu,” alisema Tsuma Madafu.

Aliongeza: “Tuna orodha yenye majina ya watu waliofaidika na ploti hizo ilhali mpango wa kutulipa fidia haujakamilishwa”.

Mkazi mwingine, Ali Mwadeje alisema wao kama wakazi wa Tsuza wamejawa na wasiwasi kutokana na hali kwamba NLC haijawalipa ridhaa na idadi kubwa ya wenyeji kuachwa nje katika mpango wa ugavi wa ploti.

“Wakati wale walioathiriwa na awamu ya kwanza ya ujenzi wa barabara ya Dongo Kundu, kulikuwa na shughuli nyingi ya uhamasisho. Lakini katika awamu ya pili na tatu wakazi hawapewi habari zozote kuhusu mipango ya ulipaji fidia. Na tunashangaa kugundua kuwa wavuvi na waendeshaji boti katika ufuo wa Mkupe hawajajuimishwa kwenye orodha,” alisema Bw Mwadeje.

Wakazi sasa wanatishia kumzuia mwanakandarasi kuendelea na mradi huo ikiwa malalamishi yao hayatashughulikiwa kwa njia ya kuridhisha.

“Tumeona matingatinga na mitambo mingine katika eneo la mradi lakini kuna masuala kadhaa ambayo hayajashughulikiwa. Hii ndio maana tumeapa kuzuia utekelezaji wa mradi huu hadi malalamishi yetu yatakaposhughulikiwa,” akasema Masoud Mohammed, mkazi wa eneo la Gandi.

“Tunaunga mkono mradi huu lakini hatufai kuchezewa shere,” akaongeza.

Awamu ya pili ya mradi huo inajumuisha ujenzi wa barabara ya safu mbili ya umbali wa kilomita 8.96, ambao unatarajiwa kuanza mwezi huu.

Kutakuwa na makutano ya barabara katika barabara kuu ya Likoni-Lunga Lunga na madaraja mawili yatajengwa, moja katika eneo la Mwache- la urefu wa mita 680 na lingine katika eneo la Mteza, la urefu wa kilomita mbili.

Mradi huo, utakaogharimu Sh25 bilioni, umeidhinishwa na afisi ya Mwanasheria Mkuu na tayara kampuni ya Fujita Corporation kutoka Japan itaweka vifaa vyake katika eneo la mradi. Wakati huo huo, ujenzi wa awamu ya tatu ya mradi wa barabara ya pembeni ya Dongo Kundu kwa gharama ya Sh30 bilioni na ujenzi wa eneo la kiuchumi unakabiliwa na changamoto za ulipaji ridhaa kwa watakaopokonywa ardhi.