Habari Mseto

Wito mikutano ya Tangatanga na Kieleweke izimwe

June 29th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

NA TITUS OMINDE

MASHIRIKA ya kijamii kutoka North Rift, yanataka serikali kusitisha mikutano ya kisiasa ya makundi ya Tangatanga na Kieleweke.

Mashirika hayo yanataka makundi hayo kupigwa marufuku hadi uchunguzi kuhusiana na madai ya njama ya kumuua Naibu Rais William Ruto unaoendelea ukamilike na ukweli kubainika.

Viongozi wa mashirika hayo walisema mikutano ya wanasiasa kutoka makundi hayo inatumika kueneza hotuba za chuki miongoni mwa Wakenya na imechangia madai ya kuwepo kwa njama ya kumuua Dkt Ruto.

Mkurugenzi mkuu wa shirika la kutetea haki za kibinadamu la Centre for Human Rights and Democracy, Bw Kipkorir Ng’etich alisema wanasiasa kutoka mirengo yote wanatumia mikutano hiyo kuendeleza siasa za chuki na uhasama miongoni mwa Wakenya wa matabaka mbalimbali.

Bw Ng’etich alisema joto la kisiasa ambalo liko nchini kwa sasa lina uwezo mkubwa wa kuchochea ghasia.

Mwanaharakati huyo alionya kuwa iwapo hali hiyo haitadhibitiwa huenda kukashuhudiwa ghasia za kisiasa kama ilivyokuwa mwaka wa 2007 /2008.

“Wanasiasa kutoka mirengo ya Kieleweke na Tangatanga wameanza kueneza uhasama ambao una uwezo mkubwa wa kuleta ghasia nchini. Mikutano hii yapaswa kuharamishwa na kupigwa marufuku hadi 2022,” alisema Bw Ng’etich.

Msimamo wake uliungwa mkono na mkurugenzi wa shirika la Centre for Human Rights and Mediation Bw Nick Omito ambaye alisema mvutano wa kisiasa kati ya Kieleweke na Tanga Tanga inarudisha nyuma maendeleo nchini.

Kurekebisha hali

Bw Omito alitaka Rais Uhuru Kenyata na Naibu wake Dkt William Ruto kujitokeza na kurekebisha hali iwapo wanataka kuafikia malengo ya ajenda ya maendeleo kwa pamoja.

“Iwapo Rais na naibu wake wanapenda kuafikia malengo ya ajenda ya nne ya maendeleo ni sharti wapige marufuku wafuasi wao kushiriki katika mikutano ya kisiasa chini ya makundi ya Kieleweke na Tangatanga,” alisema Bw Omito.

Kwa pamoja mashirika hayo yanataka uchunguzi wa kina kufanywa kuhusiana na madai ya kuwepo kwa njama ya kumuua Dkt Ruto.