• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 3:55 PM
Wito sekta ya juakali ipigwe jeki kikamilifu

Wito sekta ya juakali ipigwe jeki kikamilifu

Na LAWRENCE ONGARO

KUNA haja ya kuwapiga jeki walio katika sekta ya juakali kwa lengo la kuinua biashara zao.

Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina, amekuwa akisisitiza umuhimu wa kuwapa nafasi walio katika sekta hiyo ili waweze kuuza bidhaa zao hapa nchini.

“Bidhaa kama njiti za kiberiti na kichokonoo huwa vinaagizwa kutoka nchi za nje kama China, lakini hata sisi hapa nchini tunaweza tukawapatia vijana wetu nafasi ya kujiundia bidhaa na baadaye kuziuza hapa kwetu,” alisema Bw Wainaina.

Aliyasema hayo mwishoni mwa wiki mjini Thika alipokuwa akikagua miradi ya maendeleo.

Alisema kuna wakati amependekeza mswada bungeni ya kutaka serikali itoze hata mara tatu na zaidi bidhaa zinazoingizwa hapa nchini.

“Hata mwaka 2019 wafugaji wengi wa kuku na wafugaji wa ng’ombe waliathirika vibaya sana. Wauzaji wa mayai na maziwa walipata hasara kubwa kutokana na bidhaa hizo kuagizwa kutoka mataifa jirani,” alisema Bw Wainaina.

Bw Nelson Gaichuhie ambaye ni katibu wa usimamizi katika wizara ya ustawi viwanda alipendekeza wanajuakali wapewe nafasi ya kuunda vifaa kama vitanda na toroli, na kuzitafutia soko.

“Hawa watu wa juakali wana umuhimu wao katika uchumi wa nchi hii. Kwa hivyo, ni vyema serikali ifanye juhudi kuona ya kwamba wanapewa msaada wa kifedha na serikali,” alisema Bw Gaichuhie.

Alisema uchumi wa nchi utakuwa tu “wakati tutaenzi bidhaa zetu za hapa nchini.”

“Ni vyema kufuata wito wa ‘Kujenga Kenya na Kununua kenya’. Tukifuata wito huo bila shaka uchumi wetu utaimarika pakubwa,” alisema Bw Gaichuhie.

Alisema viwanda vitatu muhimu hapa nchini vya kushona nguo kama Rivatex cha Eldoret, Kicotex cha Kitui, na Thika Cloth Mills ( TCM), vitaimarisha uchumi wetu.

Alisema serikali itanufaika pakubwa kutokana na kuwepo kwavyo “kwa sababu vinaunda bidhaa za hapa kwetu nchini.”

You can share this post!

EPL: Aubameyang aongoza Arsenal kuwateremsha Watford daraja

Wawekezaji sekta ya utalii wadai wito wa Balala hauna...

adminleo