Wito wakulima wachukulie viwavi hatari hatua nyingine
NA GEOFFREY ONDIEKI
Watafiti wa kilimo kutoka kampuni ya Dekalb wamewasihi wakulima wa mahindi kutoka Bonde la Ufa kukumbatia mbinu mbadala kukabiliana na viwavi jeshi ambao wamekithiri eneo hilo.
Bw Robert Letich kutoka kampuni ya Delkab alisema kuna haja ya wakulima kukumbatia njia mbadala ikizingatiwa viwavi jeshi wamesababisha hasara kubwa kwa miaka ya hivi punde.
Alisema kuwa matumizi ya njia za pamoja ikiwemo mzunguko wa mazao ni muhimu kwa sababu wadudu hawa wanavamia aina moja ya mimea.
Bw Leitich aliongeza kuwa wakulima hasa wa mahindi wanastahili kujifunza kukuza mimea ambayo inaweza kustahimili magonjwa na wadudu, mbali na udhibiti wa kibayolojia wa wadudu.
“Wakulima wanastahili kuzingatia mbinu nyingine muhimu kando na udhibiti wa moja kwa moja wa wadudu,” alisema Bw Leitich.
Bw Leitich alionya wakulima kuwa matumizi ya mara kwa mara ya kemikali yanaweza kuchangia viwavi jeshi kukuza ukinzani.
“Wakati mwingine wakulima hutumia dawa aina moja mara kwa mara na hivyo kufanya viwavi jeshi kuzoea dawa,” aliongeza.
Kulingana na Bw Leitich, mazoea ya wakulima yanaweza kuchangia wadudu kukithiri.
Alisema kuwa wakati mwingine wakulima hawazingatii kutumia kiwango cha kipimo kinachostahili kwa kila mmea. Bw Leitich alihoji kuwa ili kuangamiza viwavi jeshi sharti mkulima anyunyize dawa kwa kila mmea na sio kunyunyiza nasibu kama wakulima wengi wanavyofanya.
“Wakati mwingine ukosefu wa ujuzi huchangia kukithiri kwa wadudu hawa.Sheria za msingi za matumizi zinastahili kufuatwa ifaavyo ili kuangamiza wadudu,” alisema.
Mtaalamu huyo wa kilimo alikiri kuwa wakulima wengi katika maeneo ambayo yameathirika wanashauriwa vibaya kuhusu matumizi ya pembejeo na viafaa vya kunyunyiza dawa. Kwa mfano, kunyunyiza mimea na nozeli zenye kasoro, hutawanya tu wadudu badala ya kuwaangamiza.
Mazoea mengine ambayo huchangia uvamizi wa viwavi jeshi ni pamoja na kuchelewa kupanda mimea. Alisema kuwa mimea changa ya mahindi huvutia nondo wa kike ambao huzaana haraka.
“Wakulima wanafaa kukoma kupanada mimea wakiwa wamechelewa. Wakati nondo wanatafuta mahali mwafaka pa kuzaana, huvutiwa na mimea changa ya mahindi iliyoko karibu,” aliongeza Bw Leitich.
Katika sehemu zingine za Bonde la Ufa, utafiti unaonesha kuwa viwavi jeshi wanakinzana na dawa za wadudu ambazo zinatumiwa na wakulima sehemu hizo.
Kwa mfano, baadhi ya wakulima wa mahindi pale Solai katika kaunti ya Nakuru watoa lalama zao mara kwa mara kuhusu uvamizi wa viwavi jeshi ambao umekithiri.
Wakizungumza na Taifa Leo, walisema kuwa ekari kadhaa za mimea ya mahindi imeharibiwa na juhudi zao kupigana na wadudu zimeambulia patupu.
Bi Rachel Alumasa ambaye ni mmoja wa wakulima eneo hilo, alionyesha hofu kuwa ekari yake moja iko katika hatari ya kuliwa na wadudu hao hatari.
“Nimejaribu kunyunyiza dawa aina tofauti lakini wadudu bado wanaendelea kula mimea. Ninahofia kupata hasara kwa sababu wadudu wanazidi tu kuvamia,” alisema Bi Alumasa.
Aliongeza kuwa amepoteza matumaini ya kupata mavuno yake ya kawaida ya magunia 40 kwa sababu sehemu kubwa ya mimea imeharibiwa.
“Ekari yangu moja ya mahindi imevamiwa sana na hawa wadudu na ninahofia kutopata mavuno ya kutosha,” alisema.