Wizara ya Ardhi yasikiliza malalamishi ya wakazi wa Kiang'ombe
Na LAWRENCE ONGARO
WAKAZI wa kijiji cha Kiang’ombe, Thika, wanataka serikali kuingilia kati ili kuona kwamba wanalindwa dhidi ya kero ya unyakuzi wa ardhi yao ya ekari 95.
Afisa katika afisi ya Ardhi, Bw Gedion Mung’aro, alizuru kijiji cha Kiang’ombe, na kuchukua malalamishi ya wakazi hao wapatao 540 kuhusu unyakuzi huo wa ardhi.
Kulingana na wakazi hao kuna bwanyeye mmoja mwanamke ambaye amekuwa tisho kubwa katika eneo hilo.
“Sisi kama wakazi wa hapa tumekuwa tukipewa vitisho na kufurushwa kwa lazima na mmoja wa wanyakuzi ambapo hata hivi majuzi alifurusha wakazi kadha na tayari ameanza shughuli za ujenzi mahali hapo,” alisema mmoja ambaye ni mdau muhimu katika kamati ya maskwota wanaoishi eneo hilo.
Bw Mung’aro aliwahakikishia uwazi katika uchunguzi wao akisema iwapo mshukiwa huyo atapatikana kuwa amenyakua ardhi hiyo bila stakabathi halali, bila shaka serikali itapambana naye inavyostahili.
“Mimi nimezuru hapa kujua ukweli wa mambo na kwa hivyo msiwe na hofu yoyote. Tutafanya uchunguzi wetu halafu ukweli wa mambo utabainika,” alisema Bw Mung’aro.
Nguvu za serikali
Alisema vyeti vya umiliki wa ardhi hiyo kama sio halali vitatwaliwa na serikali mara moja, na hakuna yeyote aliye na nguvu kuliko serikali.
Alitaka kamati ya maskwota hao ifike katika afisa kuu ya Ardhi House, jijini Nairobi mnamo tarehe 11 Machi, 2019, na stakabadhi zote muhimu ya ardhi hiyo ili wajue ukweli wa mambo.
Baadaye pia kamati hiyo itafanya mkutano mwingine Machi 13, 2019, na kamati ya ardhi ya Seneti ili kusikiza malalamishi yao.
Bw Mung’aro aliwahakikishia wakazi hao kuwa tayari serikali imefanya mabadiliko makubwa kwa maafisi 600 wa ardhi ambao watapelekwa katika wizara tofauti za hapa nchini.
“Hiyo ni ishara tosha kuwa serikali iko macho na inafuatilia matukio yote yanayoendelea katika idara tofauti. Kila afisa anaweza hudumu kwa wizara yoyote ile,” alisema Bw Mung’aro.
Alikuwa ameandama na Naibu Kamishna wa Thika Magharibi Bw Douglas Mutahi, maafisa wakuu wa serikalini pamoja na msaidizi wa Mbunge wa Thika Bw John Mwangi.
Jambo lingine lililoshangaza watu ni kwamba eneo lililotengwa kujengwa kituo cha polisi la ekari 10 pia limenyakuliwa tayari huku kituo cha polisi kikiwa kimejengwa kwa nusu ekari pekee.