• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 6:55 PM
Yabainika mmoja wa watoto sio wa mbunge

Yabainika mmoja wa watoto sio wa mbunge

Na RICHARD MUNGUTI

ALIYEKUWA Mbunge wa Matungu, marehemu Justus Murunga Makokha ndiye baba wa mtoto mmoja kati ya wawili wa mwanamke aliyekuwa akimuuzia uji jijini Nairobi.

Uchunguzi wa DNA uliofanywa katika maabara ya Crystal Lab Pathologists ulibaini kuwa Murunga ndiye baba ya mtoto huyo mwenye umri wa miaka mitatu.

Lakini sampuli zilizochukuliwa kutoka kwa mtoto wa pili wa mwanamke huyo zilionyesha baba yake sio marehemu Murunga.

Ripoti hiyo ya uchunguzi ilitolewa Jumatatu na madaktari wawili Dkt M. Mwangi na Dkt P. M. Maturi waliopima sampuli zilizotolewa kutoka kwa mwanamke huyo, watoto wake wawili na mwili wa Bw Murunga.

“Baada ya kukagua sampuli, asilimia 99.9 za DNA za msichana zinafanana na za Murunga lakini za mvulana hazifafani,” ilisema ripoti.

Kufuatia ufichuzi huo, wakili Danstan Omari alisema atawasilisha kesi mahakamani ili msichana huyo arithi mali ya Murunga pamoja na watoto wengine wa mwanasiasa huyo aliyeaga dunia Novemba 14, 2020.

Sheria inamruhusu hata mtoto wa kwanza awe akipokea msaada kutoka kwa mali ya Murunga kwa vile mbunge huyo alikuwa akimtunza tangu azaliwe 2013.

Katika kesi iliyowasilishwa kortini na Bw Omari, mwanamke huyo alisema kuwa Murunga ndiye alikuwa baba ya watoto wake wawili wenye umri wa miaka saba na mitatu mtawalia.

Bw Omari alifaulu kusimamisha mazishi ya mbunge huyo hadi sampuli zitolewe kwa mwili wa mbunge huyo kupimwa katika maabara kuthibitisha madai ya mwanamke huyo.

Kwenye kesi hiyo, mlalamishi alieleza kwa undani jinsi alivyokutana na Murunga 2012 akiwa anauza uji, magimbi – nduma – na viazi vitamu katika eneo la Ruai.

Wakati huo mwanasiasa huyo alikuwa msimamizi wa kampuni ya kuuza mashamba ya Embakasi Ranching.

“Tulianza urafiki na Murunga 2012 na mnamo 2013 nikapata uja uzito nikajifungua mtoto wa kwanza mvulana na Murunga,” alisema Bi Wambiri katika ushahidi aliowasilisha mahakamani.

You can share this post!

COVID-19: Visa 163 vipya, wagonjwa 6 wafariki

Wahudumu wa afya, wagonjwa wamlilia Uhuru