• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
Yabidi vyeti 400 vya ardhi vibatilishwe

Yabidi vyeti 400 vya ardhi vibatilishwe

Na SAMUEL BAYA

WIZARA ya ardhi ililazimika kurudisha zaidi ya hati 400 za kumiliki ardhi ilizonuia kuwapa wakazi wa Kwale baada ya mbunge wa Kinango Bw Benjamin Tayari kulalamika kuwa shughuli hiyo haikufanyika kwa njia ya haki.

Waziri msaidizi wa ardhi, Bw Gideon Mung’aro, aliambia Taifa Jumapili kwenye mahojiano kwamba wizara ilikuwa tayari kugawa hati hizo lakini bunge likasimamisha zoezi hilo.

“Hata tulikuwa tumeanza mipango ya kutoa hati hizo lakini waziri wa ardhi Bi Faridah Karoney akaitwa bungeni. Awali mbunge wa sehemu hiyo alikuwa amelalamika bungeni kwamba zoezi hilo halikufanyika kwa njia ya haki na lilifaa kurudiwa,” akasema Bw Mung’aro.

Alisema kuwa kwa sababu suala hili liko bungeni, wao watafanya watakavyoelekezwa na bunge kufanya.

“Tunasubiri bunge litupatie mwelekeo na sisi hatutasita kutekeleza kazi yetu. Hatujakataa kutoa hati hizo kwa wakazi hao,” akasema Bw Mung’aro.

Akiongea na Taifa Jumapili Bw Tayari alisema aliomba usaidizi wa bunge baada ya kampuni moja kudai inamiliki sehemu ya ardhi ya wakazi.

“Eneo la Maji ya Chumvi ni mpango wa makazi na hakuna kampuni ambayo inafaa kupata ardhi isipokuwa wakazi wenyewe. Jambo ambalo tunataka kujua ni je, ni kwa njia gani kampuni hiyo ilipata ardhi hiyo? Kwa sababu hiyo niliomba bunge lisimamishe zoezi hili ili ardhi hiyo ipimwe upya,” alisema Bw Tayari.

Naye Gavana wa Kwale, Bw Salim Mvurya kupitia kwa msemaji wake Daniel Nyassy alisema kuwa serikali ya kaunti itahakikisha kwamba wenyeji halisi ndio watapatiwa ardhi eneo hilo.

“Lazima tuhakikishe kwamba wenyeji halisi ndio watanufaika na hiyo ndio maana zoezi la kuchuja hati miliki linafaa kufanywa upya na kwa utaratibu zaidi ili wenyeji wasidhulumiwe,” alisema Bw Nyassy.

Aidha, Bw Nyassy alisema kuwa mwaka 2018, Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) ilizuia utoaji wa hati hizo mpaka pale uchunguzi kamili utakapofanywa kubaini walionufaika.

Wiki iliyopita, baadhi ya wakazi walielezea hofu yao kwamba huenda ardhi hiyo ikanyakuliwa na mabwenyenye baada ya hati hizo miliki kurudishwa Nairobi.

Wakazi hao wakiongozwa na Mzee Dzomo Magongo walisema hatua ya kusimamisha utoaji wa hati hizo ni mpango wa baadhi ya wanasiasa kuwapokonya ardhi yao na kuuuzia matajiri.

  • Tags

You can share this post!

Kamket apuuza madai ya njama ya kumuua Ruto

MWANASIASA NGANGARI: Ngala alitamba katika siasa za Ukambani

adminleo