• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
Yafichuka MCA mfu alilipwa marupurupu kwa ‘kuzuru’ Uganda

Yafichuka MCA mfu alilipwa marupurupu kwa ‘kuzuru’ Uganda

Na DICKENS WASONGA

UCHUNGUZI wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kuhusu ziara tata ya madiwani wa Siaya nchini Uganda ulichukua mkondo wa kushtua baada ya kubainika kuwa diwani aliyefariki aliorodheshwa miongoni mwa waliosafiri.

Imebainika kuwa madiwani hao 41 walidanganya kwamba walisafiri hadi Jinja, Uganda ndiposa walipwe marupurupu.

Waliwasilisha paspoti zao kwa afisi ya idara ya uhamiaji katika mjini wa mpakani wa Busia na wakarejea makwao bila kuhudhuria warsha nchini Uganda.

Lakini kujumuishwa kwa jina la Joanes Andiego Odongo katika orodha ya madiwani waliosemekana kusafiri kumeshangaza hata zaidi.

Hii ni kwa sababu Odongo alifariki mnamo Mei 17, 2018 akihudumu kama diwani wa wadi ya Central Sakwa. Vilevile, alikuwa kiranja wa wengi katika bunge la kaunti ya Siaya.

Nafasi yake ilijazwa na Bw Charlton Andiego aliyeshinda katika uchaguzi mdogo uliofanyika miezi mitatu baadaye.

Bunge la kaunti sasa limejitetea likidai kuwa hitilafu “ya majina ya madiwani walioteuliwa kwa safari ya Uganda.”

Hata hivyo, stakabadhi za malipo zilizowasilishwa na afisi ya karani wa bunge hilo zinaonyesha kuwa marehemu alisafiri na akalipwa marupurupu zote.

Kulingana na stakabadhi hiyo iliyotayarishwa mnamo Januari 21, 2019, jumla ya madiwani 43 walikuwa wamepangiwa kuhudhuria warsha hiyo ya mafunzo katika ukumbi wa shirika la Lake Victoria Fesheries Organisation (LVFO) jijini Jinja kutoka Februari 1, hadi 15.

Ndani ya kipindi hicho, madiwani walipaswa kulipwa Sh136,144 kila moja kama marupurupu ya matumizi pamoja na Sh10,000 kama marupurupu ya usafiri.

Naye Spika wa bunge hilo George Okode alipaswa kutia kibindoni kitita cha Sh184,346.

Ufisadi wachukua mwelekeo mpya

Mnamo Alhamsi msemaji wa EACC Yasin Amaro aliambia Taifa Leo kwamba inasitikisha kuwa ufisadi umechukua mwelekeo mpya kutoka wale wanaoorodheshwa kama wafanyakazi hewa hadi wasafiri wafu.

“Kando na vianzo vyetu vya habari, EACC ilitegemea stakabadhi zinazohusiana na suala linachunguzwa kutoka kwa watu binafsi na mashirikisha yanayochunguzwa,” akasema.

Lakini tulipomfikia kwa njia ya simu, Bw Okode alidai kuwa orodha hiyo ilikuwa na kasoro na anaisuta EACC kwa kujishughulisha na “masuala yasiyo na maana.”

“EACC inaibua drama isiyo na maana. Je, wana ushahidi kuwa jina la MCA lilitumiwa kutoa pesa. Je, wana ushahidi kuonyesha kuwa jina lake lilijumuisha katika orodha ya madiwani waliosafiri?” Spika huyo akauliza.

EACC imewaita madiwani hao 41 wa Siaya ili watoe maelezo kuhusu ziara hiyo iliyogubika na utata.

  • Tags

You can share this post!

DAU LA MAISHA: Mafanikio ni bidii ya mtu, yake sasa inalipa

SHANGAZI AKUJIBU: Sili silali baada ya mpenzi kukataa...

adminleo