Habari Mseto

Yaibuka aliyechimba barabara peke yake alikuwa mhalifu sugu

June 12th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na NDUNGU GACHANE

MWANAMUME mwenye umri wa miaka 45 aliyegonga vichwa vya vyombo vya habari kwa kuchimba barabara ya kilomita 2 peke yake, alikuwa mraibu wa dawa za kulevya aliyebadilika na sasa ni shujaa anayetambuliwa na jamii, mashirika ya kibiashara na wasamaria wema.

Bw Nicholas Muchami kutoka kijiji cha Kaganda, eneobunge la Kiharu Kaunti ya Murang’a alichimba barabara kwenye eneo la mlima akitumia vifaa vyake vya shambani ili kusaidia wazee, wagonjwa, wanawake na wanafunzi waliokuwa wakitembea mwendo wa kilomita nne kufika sokoni na shuleni.

Bila kutarajia malipo yoyote kutoka kwa jamii, hatua ya Bw Muchami ilisifiwa na umma na kumfanya atambuliwe na jamii na nchi kwa jumula.

Mwanamume huyo ambaye awali alikuwa akidharauliwa na jamii kwa sababu ya rekodi yake ya kufungwa jela miaka miwili kwa kumvunja mkono baba yake alipokataa kumpa parachichi mwaka wa 2005 na kwa kuvuta bangi mwaka wa 2015 hakufikiria kuwa siku moja ataheshimiwa na jamii.

Muchami ambaye alibadilika, aliamua kusaidia jamii bila kutarajia malipo au kutambuliwa na yeyote lengo lake likiwa ni kusaidia watu ili waache kutembea mwendo mrefu.

Akiongea baada ya kupokea ng’ombe wa maziwa na lishe ya miezi sita kutoka kwa benki ya ABC mnamo Jumanne, Bw Muchami alisema anamshukuru Mungu.

“Nilikuwa nikifuta bangi na kutumia vitu vibaya lakini tangu nilipobadilika na kuokoka katika kanisa la ACK Kaganda, Mungu amekuwa nami, nilichimba barabara hiyo bila kujua kile ambacho kingetendeka lakini baadaye juhudi zangu zimenifanya maarufu kwa kumiliki ng’ombe wawili wa maziwa, kupatiwa lishe na maji ya mfereji,” alisema Bw Muchami.

Bw Muchami ambaye kwa wakati huu ni mlinzi katika shule ya msingi ya Kaganda, alisema hakuwa ameoa kwa sababu ya rekodi yake uhalifu na umasikini lakini sasa yuko tayari kupata mke wa kutunza mali aliyopatiwa na Mungu.