'Yaliyojadiliwa kwenye kongamano la wanaume pekee mjini Eldoret'
Na WYCLIFF KIPSANG
WANAUME wamelipa ada ya kiingilio ya Sh2,000 kila mmoja kuhudhuria Kongamano la Wanaume lililohutubiwa na mwanasiasa mkongwe Jackson Kibor mjini Eldoret, Kaunti ya Uasin Gishu.
Waandalizi wa kongamano hilo lililofanyika Jumatatu katika hoteli ya Noble wamesema mkutano huo ulilenga kuwawezesha wanaume kujiamini.
Bw Kibor, 85, ambaye alikuwa mmoja wa watu mashuhuri waliohutubia kongamano hilo ameelezea masikitiko yake kutokana na ongezeko la vijana wanaoangamia kutokana na matumizi ya mihadarati na magonjwa yanayosababishwa na mtindo wa maisha.
“Siri ya kuishi miaka mingi ni kula chakula cha kitamaduni. Ukienda katika shamba langu, hutaamini kwamba ni la mtu mzee kama mimi,” amesema Bw Kibor.
Amesema vijana wengi wamekuwa wazembe na sasa wanategemea kurithi mali kutoka kwa wazazi wao badala ya kufanya kazi kwa bidii.
“Unataka kula ya nani kama hutaki kutafuta yako?” amesaili Mzee Kibor ambaye hivi majuzi alishtaki mwanawe kwa kudai sehemu ya mali yake.
Amesema alibadili uamuzi wake wa kuwagawia urithi watoto wake baada ya mmoja wa wana wake aliyekuwa akijipatia mapato ya Sh4 milioni kutokana na kilimo cha mahindi, kufariki kutokana na ubugiaji wa pombe.
Desemba 2018 mahakama ya Eldoret iliruhusu Kibor kuachana na mke wake aliyeishi naye kwa kipindi cha miaka 42 kwa wakati huo.
Bw Kibor amewashauri vijana ambao ndoa zao zinakumbwa na msukosuko kutalikiana na wake zao badala ya kuumia kimyakimya.
Uwekezaji
Waliohudhuria pia wamepewa mafunzo kuhusu uwekezaji, kuboresha ndoa zao na kuimarisha uhusiano wao na wanawake.
“Wanaume wanaendelea kupoteza ushaiwishi wao katika familia na jamii. Wanafaa kujikakamua na kujiinua kiuchumi,” amesema Askofu (Mstaafu) Jackson Kosgey, ambaye pia amehudhuria kongamano hilo.
Baadhi ya wanaume wameambia Taifa Leo kuwa wake zao walikuwa wamekerwa na hatua yao kuhudhuria kongamano hilo kutokana na hofu kwamba wangepotoshwa na Bw Kibor ambaye amekuwa akitalikiana na wake zake mara kwa mara.
Mzee Kibor hivi majuzi alizua kizaazaa mjini Eldoret alipokatakata mnyororo uliotumiwa na askari wa Kaunti ya Uasin Gishu kufunga gurudumu la gari lake.
Gari lake aina ya Toyota V8 la thamani ya mamilioni ya fedha, lilifungwa na askari hao kwa kukataa kulipa ada ya kuegesha ya Sh100.
Mnamo Februari 2019 watumiaji wa mitandao ya kijamii walidai kuhudhuria ‘kongamano hewa’ la wanaume ili kuhepa gharama za siku ya wapendanao ya Valentino ambapo walisema Bw Kibor alikuwa miongoni mwa wazungumzaji wakuu.