Yaya alia kwa kuuza pete ya Sh689, 000 kwa Sh4, 000 pekee
MJAKAZI mwenye umri wa miaka 28 Jumatatu, Agosti 12, 2024 alilia kwa uchungu ndani ya Mahakama ya Milimani baada ya kupatikana na hatia ya kuiba pete ya dhahabu ya mwajiri wake na kuiuza kwa Sh4, 000 pekee, thamani yake ikikadiriwa kuwa Dola za Amerika (USD – $) 5, 300 sawa na Sh689, 000.
Violet Ndukweh Lijoodi aliyefikishwa mbele ya hakimu mkazi Mahakama hiyo Rose Ndobi alijiona hafai alipoungama makosa yake na kuomba msamaha huku akilia kwa uchungu.
Ndukweh alikiri kwamba alimwibia mwajiri wake Norah Mitchell Were pete hiyo ya thamani kuu na kuiuza kwa Sh4, 000 katika soko la Kawangware.
Mahakama ilielezwa kuwa Bi Were ni Muuguzi anayefanyakazi nchini Australia.
Muuguzi huyo alikuwa nchini kwa likizo.
Alienda kuishi katika mtaa wa Runda na mtu wa familia yake pamoja na watoto wake wawili.
“Bi Were alifika nchini Kenya kwa likizo pamoja na watoto wake wawili. Aliomba atafutiwe mboch (yaya) kumsaidia katika kazi za nyumba. Alitafutiwa Ndukweh aliyemwajiri kuanzia Julai 1, 2024,” hakimu alifahamishwa na kiongozi wa mashtaka.
Kati ya Agosti 3 na 8, 2024 hakimu alielezwa Ndukweh alipewa ruhusa kupumzika.
Bi Were alifungua mfuko alipokuwa ameweka pete yake ya thamani kuu lakini hakuipata.
Mshtakiwa aliporejea kutoka ruhusa alihojiwa na kukiri ndiye aliiba pete hiyo.
Polisi walijulishwa na kumtia nguvuni mshtakiwa.
Ndukweh aliwapeleka polisi hadi kwa duka la Francis Mwima ambaye aliinunua pete hiyo kwa bei ya Sh4 ,000.
Polisi hawakuipata hata baada ya kupekua pekua kila mahala kwa duka la mfanyabiashara huyo lilioko mtaani Kawangware.
Akijitetea huku akilia kwa uchungu mshtakiwa aliomba msamaha.
Akilia kwi kwi kwi alisema; “Naomba hii mahakama msamaha. Pia namuomba Mama Norah msamaha. Sikujua pete niliyoiba ilikuwa na thamani kuu kwake. Aliniambia ikiwa Sh4, 000 ni kitu basi zinisaidie.”
Ndukweh alisema alionyeshwa mahala pa kuuza pete hiyo na msichana rafikiye kwa jina Harriet.
Mjakazi huyo aliungama kwamba alikusudia pesa hizo atumie baba yake mzazi ambaye ni mgonjwa hospitalini.
Pia, aliomba korti msamaha huku akiungama “Nina watoto watatu na hakuna mtu wa kuwasaidia ila ni mimi tu. Wazazi wangu ni wakongwe na hawana mapato.”
Yaya huyo aliendelea kueleza korti kwamba ameghairi matendo yake.
Kabla ya kupitisha hukumu, hakimu aliagiza idara ya urekebishaji tabia imhoji mshtakiwa, watu wa familia yake na mwajiri wake Bi Were ibainike tabia yake na pia ikiwa alikuwa amejiingiza kwa maisha ya uhalifu hapo awali.
Hukumu itatolewa mnamo Septemba 5, 2024.
Kuhusu Mwima, hakimu alimwamuru alipe dhamana ya Sh1 milioni na mdhamini mmoja ama pesa taslimu Sh500, 000.
Mwima aliomba apewe video za CCTV za makazi ya Runda alikokuwa akifanya kazi mshtakiwa.
Lakini ombi hilo halikukubaliwa, hakimu akisema endapo upande wa mashtaka utazitegemea kama ushahidi atapewa na endapo hazitatumika basi hatapewa.
Aliamriwa azuiliwe gerezani hadi pale atakapolipa.