Habari MsetoSiasa

Zaidi ya wanasiasa 10 wagura ODM na KANU, waingia Jubilee

June 5th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na Florah Koech

VYAMA vya Kanu na ODM vimepata pigo kubwa la kisiasa katika Kaunti ya Baringo, baada ya zaidi ya wanasiasa 10 kuhamia katika Chama cha Jubilee (JP). Haya yanajiri huku uchaguzi mdogo wa eneobunge la Baringo Kusini ukizidi kukaribia.

Miongoni mwa wanasiasa hao ni William Kamuren, aliyewania kiti cha Baringo Kusini kwa tiketi ya Kanu kwenye uchaguzi wa Agosti 2017 na Amos Olempaka (ODM) kutoka jamii ya Ilchamus. Wawili hao walipokelewa na Naibu Rais William Ruto wakati alizuru eneo la Marigat, Baringo Kusini.

Bw Kamuren ametangaza azma ya kuwania ubunge katika eneobunge hilo kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wake, Bi Grace Kipchoim mwezi mmoja uliopita.

Kwenye hotuba yake katika Shule ya Upili ya Marigat, Jumapili, Naibu Rais William Ruto aliahidi kufanya kazi na viongozi wote ambao wamehamia Jubilee.

“Tunawakaribisha viongozi wote katika JP, ambapo nawaahidi kwamba tutashirikiana katika kuwaunganisha wananchi ili kuwaletea maendeleo.

Ningetaka kuwahakikishia wakazi wa Baringo Kusini kwamba hatuna mwaniaji ambaye tunampendelea, kwani tunaamini katika demokrasia. Tunawakata wapigakura kumchagua mtu ambaye wanamwamini,” akasema Bw Ruto.

Jamii ya Illchamus, inayoegemea upande wa ODM pia iliahidi kumuunga mkono Bw Ruto. Aidha, ilimhakikishia kwamba tayari imekigura chama hicho kujiunga na Jubilee.

Bw Ruto aliisifia hatua hiyo, akiitaja kuwa mapambazuko mapya ya kisiasa.