Habari Mseto

Zaidi ya watu milioni moja sasa wanaugua corona duniani

April 3rd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

JUMA NAMLOLA na LEONARD ONYANGO

VIRUSI hatari vya corona vinaendelea kusambaa kwa kasi ulimwenguni, huku zaidi ya watu milioni moja wakiwa wameambukizwa.

Kufikia Ijumaa jioni, watu 1,039,158 walitangazwa kupatikana na virusi hivyo, huku zaidi ya 55,000 wakifariki. Nchini Kenya, mtoto wa kiume wa miaka sita aliongeza idadi hiyo ya waliouawa na corona kuwa watu wanne kufikia sasa.

Waziri Msaidizi katika wizara ya Afya, Dkt Mercy Mwangangi alitangaza kuwa, watu wengine 12 walithibitishwa kuambukizwa.

“Katika saa 24 zilizopita, tulipima watu 362 ambapo 12 waligunduliwa kuwa walioambukizwa ugonjwa wa corona. Kati ya hao, 11 ni Wakenya na mmoja ni raia wa Somalia. Hii sasa inafanya jumla ya walioambukizwa nchini kuwa watu 122,” akasema.

Dkt Mwangangi aliyetoa taarifa kwa niaba ya waziri Mutahi Kagwe, alisema corona ni ugonjwa hatari ambao umeathiri watu katika nchi 204 kote ulimwenguni.

“Visa vya maambukizi ya watu hao 12 vinaonyesha kuwa, Nairobi inaongoza kwa watu 7, Mombasa wawili na kaunti za Kiambu, Laikipia na Nyeri zina mtu mmoja kila moja,” akasema.

Wagonjwa hao wapya ni wanaume wanane na wanawake wanne wa umri wa kati ya miaka 28 na 68.

Kulingana na takwimu zilizokusanywa na Chuo Kikuu cha Johns Hopkins, nchi ya Amerika inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya watu walioambukizwa. Kufikia jana jioni, zaidi ya Waamerika 245,000 walikuwa na virusi hivyo.

Barani Afrika, Algeria inaongoza kwa kuwa na watu 986 waliaombukizwa ikifuatwa na Misri kwa watu 865.

Dkt Mwangangi alitangaza kufikia sasa, jumla ya watu 1,433 wamepimwa, na kuna wengine 617 walio karantini wakisubiri kupimwa. Serikali pia inawasaka watu 648 ambao walitangamana na wagonjwa hao, na huenda wanaendelea kusambaza virusi hivyo iwapo tayari wameshaathirika.

Aliwaomba MCAs katika mabunge ya kaunti waongeze juhudi katika kuwezesha vituo vya afya kukabiliana na tisho la corona katika kaunti zao.

“Si lengo letu kuingilia kazi za wawakilishi wadi kwenye kaunti mbalimbali, lakini wakati huu, jukumu kubwa tunalotarajia walitekeleze ni kufanikisha kaunti zao kujiandaa kukabiliana na ugonjwa huu, ambao sasa ni janga la ulimwengu mzima,” akasema.

Dkt Mwangangi alitoa wito huo jana huku chama cha Jubilee kikimwondoa uongozini Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kirinyaga Bw James Murang’o.

Barua iliyoandikwa na Katibu Mkuu, Bw Raphael Tuju inasema kuwa, Bw Munrang’o alipuuza ushauri wa chama na kuamua kuunga mkono juhudi za kumwondoa Gavana Anne Waiguru kabla chama hakijamaliza uchunguzi wa madai ya wanaotaka kumwondoa.

Serikali pia ilitangaza kuwa viwanda vinne vya nguo vimepewa kandarasi ya kutengeza nguo na barakoa (vitambaa vya kujikinga na maambukizi).

Waziri wa Ustawishaji Viwanda, Bi Betty Maina, alisema tayari kuna barakoa miloni moja zilizoundwa na kuidhinishwa na Mamlaka ya Kukadiria Ubora wa Bidhaa nchini (KEBS).