Habari Mseto

Zawadi ya busaa yamweka pabaya

February 13th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na BENSON MATHEKA

Mwanamume alitozwa faini ya Sh10,000 au afungwe jela miezi mitatu kwa kupatikana na mtungi wa busaa aliyopatiwa kama zawadi na mwajiri wake.

Bw Simon Mwangi aliambia Hakimu Mkuu Mwandamizi wa Kibera Barbara Ojoo kwamba alikamatwa dakika chache baada ya kupatiwa mtungi uliojaa pombe hiyo na mwajiri wake katika mtaa wa Kisimayu, Langata jijini Nairobi mnamo Februari 11 mwaka huu.

Kwa ujasiri, alieleza mahakama kwamba pombe hiyo haikuwa yake peke yake.

“Haikuwa pombe ya kuuza. Ilikuwa zawadi tuliyopatiwa na mwajiri wetu kwenda kujiburudisha baada ya kazi,” alisema.

Alisema kwamba japo ni yeye aliyekamatwa akiwa na pombe hiyo haikuwa yake peke yake. “ Wenzangu waliniambia niende kuweka kwangu tukipanga kwenda kuburudika nilipokutana na maafisa wa polisi wakanikamata,” alisema.

Bw Mwangi alisema hayo baada ya kukiri shtaka la kupatikana na pombe haramu kinyume cha sheria. Mahakama iliambiwa kwamba mnamo Februari 11, katika eneo la Kisimayu, Langata alipatikana na lita 20 za busaa akijua kwamba ilikuwa pombe haramu.

Alipoulizwa na hakimu iwapo alifahamu ilikuwa pombe haramu mshtakiwa alisema: “ Ndiyo mheshimiwa, ninajua ni pombe haramu lakini si vibaya kuitumia nyumbani ukiipatiwa kama zawadi.”

Alipoonyeshwa mtungi uliokuwa na pombe hiyo alithibitisha ni aliokamatwa akiwa nao na kusisitiza kuwa ilikuwa zawadi kutoka kwa mwajiri wao.

“Unasema mlilipwa mshahara wenu wa siku hiyo na kisha mkapatiwa mtungi wa busaa?” hakimu alitaka kujua.

“Ndio mheshimiwa, huwa ninaitumia mara kwa mara wakati wa sherehe na haijawahi kunidhuru,” alieleza.