Habari Mseto

Zoezi la kiusalama lasababishia abiria na wafanyakazi majeruhi JKIA

November 16th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

IDADI isiyojulikana ya wafanyakazi na abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) walijeruhiwa Alhamisi wakati wa majaribio ya kiusalama (security drill).

Mamlaka ya Usimamisi wa Viwanja vya Ndege Nchini (KAA) shughuli hiyo ilihusu mtu mmoja ambaye hakujitambulisha alipiga simu akitoa habari kwamba kulikuwa na vilipuzi katika uwanja huo ambao ulikuwa karibu kulipuka.

Baada ya dakika 30, mlipuko ulitokea katika kituo cha pili cha abiria (Terminal 2) na kusababisha wafanyakazi waliokuwa kazini na abiria kutoroka ili kujisalimisha.

“Mtu mmoja alipiga simu asubuhi na kutoa habari kwamba kilipuzi kilikuwa kimetegwa katika eneo moja karibu na kituo cha polisi na kilitarajiwa kulipuka wakati wowote. Na baada ya nusu saa mlipuko ulitokea katika kituo cha pili cha abiria na kupelekea kujeruhiwa kwa wafanyakazi na baadhi ya abiria,” KAA ilisema kwenye taarifa.

“Ilichukua muda wa miezi miwili kujiandaa kwa zoezi hilo na kushirikisha idara zote katika JKIA pamoja na wadau husika,” ikaongeza.

Kulingana na KAA, viwanja vyote vya ndege inapaswa kufanya majaribio kujadiria kujiandaa kwao kukabiliana na vitisho vya kiusalama.

Mnamo Jumanne Waziri wa Uchukuzi James Macharia aliwaambia wabunge kwamba usalama umeimarishwa zaidi katika uwanja wa JKIA haswa baada ya kupandishwa hadhi ya kuweza kupokea ndege za kutoka Amerika.

“Baada ya safari za ndege za moja kwa moja kutoka JKIA hadi New York Amerika kuanza mwezi jana, bila shaka hali ya usalama imeimarishwa zaidi katika uwanja huo. Mimi pamoja na waziri wenzangu kutakuwa tukifanya ziara za ghafla katika uwanja huo kukagua hali ya usalama,” Bw Macharia akawaambia wanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Uchukuzi alipofika mbele yao katika majengo ya bunge kujibu maswali kutoka kwa wabunge.