Mwanawe Museveni atishia kumfurusha balozi wa Amerika nchini Uganda
MWANAWE Rais wa Uganda Yoweri Museveni, Muhoozi Kainerugaba, amemtaka Balozi wa Amerika William Popp kumwomba msamaha kwa rais la sivyo aondoke Uganda.
Kwenye ujumbe katika mtandao wa X Jenerali Muhoozi alitaja hatua ya balozi huyo kama ya “kumkosea heshima Museveni na kuhujumu katiba ya Uganda” kama sababu ya kumtaka aombe msamaha kwa Museveni.
“Ikiwa balozi huyu wa Amerika hatamwomba msamaha mzee (Museveni) kufikia Jumatatu, Oktoba 6, asubuhi kutokana na mienendo yake ya kukiuka misingi ya kidiplomasia nchini mwetu, tutamwamuru aondoke Uganda,” akasema Ijumaa, Oktoba 4.
Jeneral Muhoozi ambaye ni mkuu wa majeshi ya nchi kavu, alisema kuwa katika siku za hivi karibuni Amerika imekuwa ikishambulia serikali ya Rais Museveni ambayo imedumu uongozini mwa miaka 38 tangu 1986.
“Hatuna shida na Amerika. Nilivyosema mara nyingi, ni nchi ambayo tunaipenda. Lakini katika siku za hivi karibu tunapata ushahidi mwingi kwamba wamekuwa wakihujumu serikali ya National Resistance Movement (NRM),” Jenerali Muhoozi akaeleza.
“Ikiwa mtu ni MJINGA kiasi cha kutushambulia hapa kwetu, ninaweza tu kuwaahidi jehanamu, uharibifu na kuangamizwa! Tutapambana nao hata kuliko Afghanistan ilivyofanya. Baba zetu walituonyesha njia, kujitolea ni bora kuliko utumwa,” aliongeza.
Kufikia Jumamosi mchana, Amerika haikuwa imejibu kauli tata zilizotolewa na Jenerali Muhoozi.
Vikwazo
Kauli hizo zinajiri wiki moja baada ya Amerika kuwawekea vikwazo maafisa wa zamani wakuu wa polisi na wa jeshi la Uganda (UPDF).
“Tunajaribu kuchanganua kauli hizo, muktadha na mazingira yalikotolewa,” afisa mmoja, ambaye aliomba jina lake libanwe, aliambia gazeti la ‘The East African’.
Mnamo Oktoba 2, Wizara ya Masuala ya Kigeni ya Amerika ilisema inawachukulia hatua maafisa wa polisi Bob Kagarura, Alex Mwine, Elwelu Womanya na Hamdani Twesigye kwa kujihusisha na vitendo vya ukiukaji mkubwa wa haki za kibinadamu.
Wizara hiyo ilisema kuwa Elwelu analengwa kwa mauaji ya kiholela yaliyotekelezwa na maafisa wa jeshi la UPDF ilhali wengine walilengwa kwa madai ya kushiriki ufisadi.
Maafisa wengine wa zamani wa usalama nchini Uganda waliowekewa vikwazo na Amerika ni pamoja na aliyekuwa mkuu wa polisi Jenerali Kale Kayihura, aliyekuwa mkuu wa idara ya ujasusi Meja Jenerali Abel Kandiho, Mkuu wa Idara ya Magereza nchini Uganda Johnson Byabashaija na mwenyekiti wa Shirikisho la Kandanda Moses Magogo, ambaye ni mumewe spika wa Bunge la Uganda.
Rais Museveni alipokea stakabadhi za Balozi Popp mnamo Septemba 2023, akimmkaribisha kama balozi wa Amerika nchini Uganda.
Uganda imekuwa na uhusiano mzuri wa kidiplomasia na Amerika, kwa zaidi ya miaka 60. Hii ni licha ya kwamba juzi, Rais Museveni alielekeza shutuma kali dhidi ya mataifa ya Magharibi.
Maafisa wa kidiplomasia huhudumu chini ya sheria ya kimataifa inatokana na Kipengele cha 9 cha Mkataba wa Vienna.
Sheria hiyo inasema kuwa nchini ambako afisa wa kidiplomasia anahudumu inaweza, wakati fulani, bila kutoka maelezo yoyote kumwamuru afisa wa kidiplomasia aondoke
Uganda inashutumu vikali vikwazo ambavyo Amerika iliwawekea maafisa hao wa usalama ikitaja hatua hiyo kama “dhuluma isiyoweza kuvumiliwa.”