10 wajeruhiwa katika fujo za uchaguzi wa ODM
UCHAGUZI wa mashinani wa chama cha ODM Jumatano ulikunbwa na vurugu katika kaunti mbili za Nyanza, tu mmoja akikamatwa na wengine zaidi ya 10 kujeruhiwa baada ya makundi mawili kukabiliana.
Katika eneo la Bondo, Kaunti ya Siaya, watu sita walijeruhiwa baada ya makundi mawili kushambuliana wakati wa uchaguzi uliofanyika katika ofisi za ODM eneo la Koyucho.
Inadaiwa kuwa kundi moja lilishuku wenzao wangelijaribu kuvuruga uchaguzi, hali iliyochochea mapigano yaliyodumu kwa muda hadi polisi walipowasili na kurejesha utulivu.
“Tumeanzisha uchunguzi wa kina kuhusu vurugu hizi. Polisi walituliza hali ili uchaguzi uweze kuendelea,” alisema Kamanda wa Polisi Bondo, Bw Robert Aboki.
Majeruhi walikimbizwa katika Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Bondo kwa matibabu.
Vurugu pia zilishuhudiwa katika eneo la Nyakach, Kaunti ya Kisumu, ambapo mtu mmoja alikamatwa akiwa na visu na mapanga.
Polisi walisema mshukiwa huyo alikuwa sehemu ya kundi kutoka Nyando lililopanga kuvuruga uchaguzi uliofanyika katika kambi ya Chifu ya Kodingo.
Aidha, mshukiwa huyo alidai kwamba kundi lao la watu watano lilitumwa na mwanasiasa fulani kuanzisha vurugu wakati wa uchaguzi. Wenzake walitoroka baada ya hasira za wananchi.
Licha ya vurugu kushuhudia maeneo kadha, uchaguzi uliendelea kwa utulivu sehemu zingine ikiwemo Nyakach.
Katika kituo cha Pap Onditi, Afisa Msimamizi wa Uchaguzi Nyakach, Bw Nehemiah Okwach, alithibitisha kuwa uchaguzi ulimalizika vyema licha ya changamoto chache za hapa na pale.
“Tumekamilisha uchaguzi wa mashinani kwa amani, isipokuwa matukio machache yaliyosababishwa na watu wachache waliotaka kuzua vurug,” alieleza Bw Okwach.