2019: Mwaka wa ahadi hewa
Na BENSON MATHEKA
MWAKA wa 2019 ulipoanza, Wakenya walikuwa na matumaini makubwa kwamba viongozi wa serikali wangewatimizia ahadi walizowapa za kuimarisha maisha yao.
Hata hivyo, mwaka 2019 unapofikia kikomo, utaacha Wakenya wakiwa katika hali mbaya zaidi kiuchumi, wakiwa wamegawanyika kisiasa na bila matumaini baada ya ahadi walizopatiwa na serikali kukosa kutimizwa.
Walitarajia kuwa viongozi wangetumia utulivu uliojiri nchini kufuatia handisheki kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga kukuza uchumi, kufanikisha Ajenda Nne Kuu ambazo zingeimarisha afya kwa kila mmoja, kufufua viwanda ili kubuni nafasi za kazi kwa vijana, kuwa na makao nafuu na chakula cha kutosha.
Kwenye hotuba yake ya kukaribisha mwaka wa 2019, Rais Kenyatta alisema serikali yake ilikuwa imeanza kutekeleza Ajenda Nne Kuu ambazo zingebuni nafasi za kazi kwa vijana.
Licha ya kuahidi vijana kazi, mwaka 2019 unakamilika huku nafasi za kazi zikiendelea kupungua baada ya kampuni nyingi kufungwa kutokana na hali ngumu ya kiuchumi.
Nafasi chache zilizopatikana serikalini zilipatiwa wazee huku vijana wakilalamika.
Hii ni kinyume na manifesto ya Jubilee ya kubuni nafasi za kazi 1.3 milioni kila mwaka katika kipindi cha pili cha utawala.
“Kujitolea kwetu kwa watu wa Kenya ni kuendelea kushirikiana na Wakenya wote kujenga misingi imara, kubuni nafasi zaidi na bora za kazi, kuboresha maisha ya kila Mkenya, kupunguza ukosefu wa usawa na kutoa Wakenya wengi kutoka lindi la umasikini,”Jubilee iliahidi katika manifesto yake.
Katika kilimo, huu ni mwaka ambao wakulima wa mahindi walivunjika moyo baada ya Bodi ya Taifa ya Nafaka na Mazao (NCPB) kukataa kununua zao lao na kuwapa pembejeo za kilimo.
Ingawa iliahidi afya kwa wote, mpango huo ungali unafanyiwa majaribio huku wagonjwa katika kaunti ulioanzishwa wakilalamika kuwa hakuna dawa na uhaba wa wahudumu wa afya.
Serikali imekuwa ikiahidi kuboresha mazingira ya kufanya biashara nchini ili kulinda na kuvutia wawekezaji ambao wangebuni nafasi za kazi kwa vijana.
Hata hivyo, kufikia Septemba 2019 zaidi ya kampuni 388 zilikuwa zimefungwa na maelfu ya watu kupoteza ajira. Kampuni kadhaa zilipata hasara zikilalamikia mazingira mabaya ya kazi pia.
Ingawa mwanzoni mwa mwaka huu, serikali iliahidi kwamba uchumi ungekua kwa asilimia 10 na zaidi, takwimu zinaonyesha ulikua kwa asilimia 4.7 mwaka huu huku Wakenya wakiendelea kulemewa na gharama ya maisha.
“Ninataka kila mfanyabiashara hata anayemiliki biashara ya rejareja kujua kwamba ndio uti wa mgogo wa uchumi wetu. Mwaka wa 2019, ninawaahidi kuwa serikali yangu itafanya kila juhudi kuchukua hatua madhubuti ili iwe rahisi kwenu kufanya biashara,” Rais Kenyatta alisema kwenye hotuba yake ya kukaribisha mwaka 2019.
Hata hivyo, unakamilika leo Jumanne wafanyabiashara wengi wakiwa wamefunga biashara zao kutokana na sera za serikali zilizofanya vigumu kuhudumu.
Kufikia Novemba 2019 shirika la taifa la takwimu (KNBS) lilisema kiwango cha gharama ya maisha kilipanda hadi 5.56 kutoka 4.95 mwezi uliotangulia.
Kwenye hotuba yake ya mwaka mpya 2019, Rais Kenyatta aliahidi kwamba kufuatia utulivu uliokuwa nchini hakungekuwa na migawanyiko ya kisiasa.
Unapokamilika leo, Wakenya wamegawanyika zaidi kisiasa huku chama chake cha Jubilee kikiwa katika makundi mawili moja likimuunga mkono na lingine likimuunga naibu wake William Ruto.
Hata ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI) alilobuni na Bw Odinga kutafuta mikakati ya kuunganisha Wakenya limezua mdahalo unaotishia kugawanya Wakenya zaidi.