HabariSiasa

2022: Raila asuasua, akosa msimamo

December 27th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

JUSTUS OCHIENG Na RUSHDIE OUDIA

KIONGOZI wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga, anazidi kukanganya wafuasi na wapinzani wake kutokana na kuonekana kukosa msimamo thabiti kuhusu kama atawania urais ifikapo 2022 au la.

Alipohudhuria ibada katika Kanisa la St Peter’s Nyamira ACK pamoja na familia yake sikukuu ya Krismasi, Bw Odinga alishangaza alipotamka kwamba hatakuwa mgombeaji urais 2022 lakini akabadili matamshi hayo haraka na kuacha watu wakijikuna vichwa.

“Sijawahi kusema nitawania urais 2022, sitawahi kutangaza hilo na mimi si mgombeaji 2022 kwa hivyo achaneni na mimi,” akaambia waumini huku akichekacheka.

Lakini aliongeza mara moja: “Tutashughulikia suala hilo wakati wake ukifika. Nipeni muda na Rais Uhuru Kenyatta tulete umoja nchini.”

Siasa kuhusu atakayechukua mahali pa Rais Kenyatta ifikapo 2022 zimezidi kunoga tangu alipotangaza ushirikiano na Bw Odinga mnamo Machi mwaka huu, kwani inadhaniwa walielewana kushirikiana uchaguzi huo utakapofika, ingawa wao hupuuzilia mbali maoni hayo.

Bw Odinga alitaka mjadala kuhusu 2022 usitishwe akidai unaathiri maendeleo wanayolenga kutimiza pamoja na Rais.

Katika ibada hiyo ya Krismasi, balozi huyo wa miundomsingi katika Muungano wa Afrika (AU), alisema msimamo aliotangaza sasa unafaa kukomesha kampeni za 2022 zinazoendelezwa wakati usiofaa, akionekana kumlenga Naibu Rais William Ruto.

Naibu Rais amekuwa akizunguka nchini kote akidai anazindua miradi ya maendeleo lakini wapinzani wake wanaona ziara hizo kuwa za kisiasa zikilenga 2022.

Wandani wa Bw Ruto jana walimkemea Bw Odinga na kusema anachezea akili za Wakenya kwa kujifanya hataki tena urais ilhali anatumia mwafaka wake na Rais Kenyatta kujiandaa kisiasa.

“Matamshi ya Bw Odinga yamenuiwa tu kupumbaza wanasiasa wasio na ujuzi,” akasema kiongozi wa wengi katika Seneti, Bw Kipchumba Murkomen.

Seneta huyo wa Elgeyo Marakwet aliongeza: “Kwa wale wanaomfahamu, Bw Odinga anachukua hatua zinazoonyesha yeye ni mgombeaji urais ingawa anatumia ujanja uliobandikwa jina ‘handsheki’.”

Seneta wa Nandi, Bw Samson Cherargei na Wabunge Oscar Sudi (Kapseret) na Caleb Kositany (Soy) walisema si siri kwamba Bw Odinga anatumia mwafaka wake na Rais Kenyatta kujiinua kisiasa na kuwania urais kwa mara nyingine.

“Anatumia ajenda kama vile kura ya maamuzi ili aendelee kuwa na nafasi kisiasa na kushikilia wafuasi wake ndiposa unaona akiyumba kuhusu msimamo wake,” akasema Bw Cherargei.