2022: Uhuru amuacha Ruto mataani
Na WANDERI KAMAU
SASA ni rasmi kuwa Naibu Rais yuko kivyake katika juhudi za kumrithi Rais Uhuru Kenyatta hapo 2022.
Hii ni baada ya Rais Kenyatta kutangaza kuwa hatamuunga mkono Dkt Ruto ama yeyote yule kwenye uchaguzi huo.
“Mungu ndiye hupeana uongozi. Yeyote atakayechaguliwa ni sawa. Mimi sijali!” akasema Rais Kenyatta Alhamisi akizungumza mjini Ruiru, Kaunti ya Kiambu.
Tangazo hilo ni usaliti kwa Dkt Ruto ikikumbukwa Rais aliahidi hadharani kuwa akikamilisha kipindi cha pili cha utawala wake atamuunga mkono kuingia Ikulu na hata kutawala miaka 10.
“Tukiingia 2017, mimi nawauliza mnipe kura zenu, nimalize mkondo wangu huu mwingine wa miaka mitano, niondoke, baton nipatie Ruto, aendelee miaka yake kumi,” akatangaza Rais Kenyatta mnamo Desemba 2, 2016 akiwa Kericho.
Lakini hizo sasa ni hekaya za abunwasi na itabidi Dkt Ruto kuweka mikakati yake akifahamu hatakuwa na baraka za mdosi wake.
Akihutubu kwenye uzinduzi wa tawi la Ruiri la kiwanda cha kutengeneza mafuta cha Bidco, Rais Kenyatta alisema kwa lugha ya Kikuyu kuwa yeye hajali kiongozi ambaye atachaguliwa katika uchaguzi huo wa 2022.
“Uria ugaathuurwo niwe ugaathurwo. Ngai niwe uui. I don’t mind.” (Yule atakayechaguliwa ndiye atakayechaguliwa. Mungu ndiye anajua. Mimi sijali).
“Uongozi utukuja na uishe. Mungu ndiye hupatiana uongozi. Kenya haiendi pahali. Serikali ya Kenya bado itakuwepo. Haina haja kuendelea kuwasumbua wananchi kwa siasa kila saa,” akasema.
Rais alionekana kuwajibu baadhi ya wanasiasa wa Rift Valley, ambao wamekuwa wakimshinikiza kueleza wazi ikiwa atatimiza ahadi ya kumuunga mkono Dkt Ruto kwenye uchguzi huo.
Baadhi ya wabunge ambao wamekuwa wakimshinikiza Rais ni Nelson Koech (Belgut), Oscar Sudi (Kapseret), Seneta Aaron Cheruiyot (Kericho), Seneta Kipchumba Murkomen (Elgeyo Marakwet) kati ya wengine. Wanasiasa hao wamekuwa wakisisitiza kuwa Rais Kenyatta anapaswa kumuunga mkono Dkt Ruto kama alivyoahidi Kericho na kwenye uzinduzi wa Chama cha Jubilee (JP) mnamo 2017.
Rais alisema hayo kwenye hafla hiyo iliyohudhuriwa pia na Dkt Ruto na kiongozi wa ODM, Raila Odinga, ambapo wote walisisitiza kuhusu haja ya viongozi kukumbatia umoja.
Uzinduzi wa kiwanda hicho pia unajiri baada ya Rais kuahirisha ziara kadhaa katika eneo la Mlima Kenya, ambapo baadhi ya viongozi wa eneo hilo wamekuwa wakimlaumu kwa kulitenga kimaendeleo.
Viongozi hao wamekuwa wakilalama kuwa Rais Kenyatta amekuwa akizindua miradi ya maendeleo katika ngome za upinzani, licha ya kutompigia kura kwenye uchaguzi wa 2017.
Rais alipangiwa kuzuru eneo hilo kati ya Mei na Aprili, lakini ziara yake ikaahirishwa ghafla kutokana na malumbano ya viongozi wa kisiasa, hasa makundi ya ‘Tanga Tanga’ na ‘Kieleweke.’
Ziara hiyo ilipangiwa kufanyika hadi mwezi Juni, lakini ikaahirishwa tena ghafla. Ilielezwa Rais alipangiwa kufanya ziara hiyo pamoja na Bw Odinga ili kuwafafanulia wakazi kuhusu handisheki.
Baadaye viongozi hao walihudhuria mazishi ya mamake aliyekuwa Mbunge wa Gatanga, Peter Kenneth katika eneo la Kirwara.