Afisi mpya ya ardhi yafunguliwa mjini Ruiru
Na LAWRENCE ONGARO
WAKAZI wa Ruiru watanufaika pakubwa baada ya kufunguliwa afisi mpya ya ardhi.
Waziri wa Ardhi Bi Farida Karoney aliyefungua afisi hiyo rasmi Jumatano alisema hatua hiyo itawapa wakazi hao kazi rahisi ya kupata hatimiliki za vipande vya ardhi.
“Nina furaha kujumuika nanyi hapa mjini Ruiru ili kushuhudia afisi mpya ikifunguliwa,” alisema Bi Karoney.
Alisema yeye akiwa ndiye Waziri wa Ardhi na yule anayemcha Mungu atahakikisha haki imetendeka kwa kila mwananchi bila kujali kabila.
Aliwalaumu maafisa wa ardhi kwa kushirikiana na mawakala ili kunyanyasa wananchi wanaotafuta hatimiliki.
“Ninafahamu vyema watu wametapeliwa pakubwa na mawakala hasa wakongwe ambao hawaelewi jinsi mambo yanavyoendeshwa kule,” alisema Bi Karoney.
Alisema wafanyakazi wote katika afisi hiyo ya ardhi watalazimika kuvalia sare za kazi na kitambulisho shingoni ili kutambuliwa na mwananchi wa kawaida.
Alisema afisi zote za ardhi zitalazimika kuhifadhi mambo yake yote kwa njia ya kidijitali.
“Tukifuata huo mtindo bila shaka ulaghai wa kutoa vyeti bandia utakwisha haraka. Hata kila kitu kitafanyika kwa utaratibu wa kuridhisha,” alifafanua Bi Karoney.
Mbunge wa Ruiru Bw Simon King’ara, alimshukuru pakubwa waziri huyo kwa kufanya juhudi ya kuleta afisi ya ardhi mjini Ruiru.
“Nina imani kuwa watu wangu ninaowakilisha watapata afueni kwa kupata afisi ya ardhi nyumbani. Mambo ya kusafiri mwendo mrefu hadi Thika, yamekwisha,” alisema Bw King’ara.
Hata hivyo alishangaza umati kwa kutaka waziri ahakikishe amepata cheti chake cha umiliki kwa ardhi aliyonunua kitambo.
“Mimi pia nilinunua kipande cha ardhi hapo awali na hadi wa leo sijapata cheti cha umiliki,” alieleza Bw King’ara.
Alisema hataki kwa vyovyote vile kujiingiza kwa siasa bali ataendelea kuchapa kazi ili kuafikia ajenda nne muhimu za Rais Uhuru Kenyatta.
Mwenyekiti wa kampuni ya kuuza mashamba ya Githunguri Ranching mjini Ruiru Bw John Maina Mburu alisema afisi hiyo mpya ni kama mkombozi kwao kwa vile wamekuwa wakizozana na kikundi kingine kuhusu utoaji wa vyeti.
“Sisi kama maafisa wa kampuni ya Githunguri tutahakikisha tunawaelekeza vyema wanachama wetu katika afisi ya ardhi iliyofunguliwa Jumatano mjini Ruiru,” alisema Bw Mburu.
Hata aliipongeza afisi mpya ya ardhi ya Ruiru kwa kuwahakikishia wananchi kuwa cheti cha umiliki kitatolewa kwa chini ya wiki moja bila kuchelewa.
Aliwahimiza wananchi wajiepushe na matapeli ambao wamewahadaa wananchi kwa muda mrefu.
Alisema kampuni ya Githunguri Ranching itafanya juhudi kuona ya kwamba kila mmoja anapata hatimiliki bila kuchelewa na kuwahimiza wajiepushe na matapeli.