COVID-19: Wizara yatangaza visa vipya 389 idadi jumla ikifika 7,577
Na CHARLES WASONGA
WATU wengine 389 zaidi walithibitishwa kuwa na virusi vya corona Jumamosi na kufikisha 7,577 idadi jumla ya maambukizi nchini Kenya.
Hii ndio idadi ya juu zaidi ya maambukizi kuwahi kuandikishwa nchini tangu Covid-19 ilipogunduliwa kwa mara ya kwanza nchini.
Kwenye taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari, Wizara ya Afya ilisema kuwa idadi hiyo ya wagonjwa wapya ilithibitishwa baada ya sampuli 4,829 kupimwa ndani ya muda wa saa 24.
Miongoni mwa watu hao 389,266 ni wa jinsia ya kiume huku 123 wakiwa wa jinsia ya kike.
“Kufikia leo (Jumamosi) jumla ya sampuli 185,035 zimepimwa tangu kisa cha kwanza cha Covid-19 kuripotiwa nchini Kenya mnamo Machi 13, 2020,” ikasema taarifa hiyo.
Na wagonjwa watano zaidi wameafriki kutokana na ugonjwa huo na hivyo kufikisha 159 idadi jumla ya maafa.
Hata hivyo, habari njema ni kwamba wagonjwa wengine 88 wamepona na kuruhusiwa kwenda nyumbani.
Kwa hivyo, jumla ya wale ambao wamepona kufikia Jumamosi ilipanda hadi kufika 2,236
Kwa mara nyingine Nairobi inaongoza kwa kuandikisha visa 248 vipya, ikifuatwa na Kajiado yenye visa 36 vya maambukizi.
Kiambu imenakili visa 27, Mombasa (23), Busia (17), Machakos (10), Migori (9), Kitui (6), Makueni (3), Uasin Gishu (3), Nakuru (2), Kilifi (2), Garissa (1), Murang’a (1) na kisa kimoja kikithibitishwa katika Kaunti ya Narok.
Katika kaunti ya Nairobi visa vya maambukizi viliripotiwa katika kama ifuatavyo; Dagoretti Kaskazini (55), Kibra (40), Langata (33), Ruaraka (17), Westlands (14), Embakasi Mashariki (13), Makadara (13), Roysambu (11) na Embakasi Kusini na Kasarani (visa 8 kila moja).
Na maeneo bunge ya Starehe, Embakasi ya Kati na Embakasi Magharibi yamesajili visa saba (7) kila moja, Embakasi Kaskazini (5) na Kamukunji iko na visa vitatu vipya.