HabariSiasa

Pwani watishia kupinga BBI

July 9th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na CHARLES WASONGA

VIONGOZI wa Pwani sasa wanatisha kupinga ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI) ikiwa mfumo mpya wa ugavi wa fedha baina ya kaunti hautawekwa kando wakisema unaipokonya eneo hilo jumla ya Sh7 bilioni.

Kwa kauli moja, magavana na maseneta kutoka kaunti zote sita za Pwani walisema hakutakuwa na haja kuweka matumaini kuwa BBI italeta usawa wa maendeleo kitaifa ilhali kwa upande mwingine wanapokonywa fedha za kufanikisha maendeleo.

Eneo la Pwani huchukuliwa kama ngome ya Kiongozi wa ODM, Raila Odinga, ambaye yuko katika mstari wa mbele kupigia debe mchakato mzima wa BBI.

Kulingana na viongozi wa eneo hilo, mfumo huo mpya unaogawanya fedha kwa kaunti 47 kwa misingi ya michango yao kwa utajiri wa nchini (GDP), utanyima Pwani fedha zinazohitaji kujiimarisha kimaendeleo baada ya kutengwa kwa miaka mingi iliyopita.

Mnamo Jumanne, maseneta sita kutoka eneo hilo walisema wako tayari kuasi vinara wa vyama vyao kupinga mfumo huo waliosema utakosesha pwani matunda ya ugatuzi.

“Hatutaunga mkono BBI, kura ya maamuzi wala miungano yoyote ya kisiasa ikiwa utekelezaji wa mfumo huo hautasimamishwa. Hili suala muhimu linahusu maisha ya watu wetu; na tuko tayari kuasi miegemeo yetu ya kisiasa kwa sababu hii,” Seneta wa Kilifi Stewart Madzayo akawaambia wanahabari katika majengo ya Bunge, Nairobi.

Aliandamana na wenzake; Mohammed Faki (Mombasa), Issa Juma Boy (Kwale), Johnnnes Mwaruma (Taita Taveta), Ali Wario (Tana River) na Anwar Oloitipitip (Lamu) kuwasilisha ujumbe huo ulioidhinishwa na magavana wao.

“Huu mfumo unakiuka hitaji la usawa katika nyanja ya maendeleo ambalo tunapania kufikia kupitia mchakato wa BBI. Kwa hivyo, mpango huo hautakuwa na maana yeyote kwetu wapwani ikiwa tutapokonywa fedha za maendeleo,” akasema Bw Faki.

Wiki iliyopita, Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho aliisihi Seneti kutupilia mbali mfumo huo mpya wa fedha akisema utahujumu ajenda za maendeleo katika eneo zima la Pwani.

“Pwani imeanza kupata maendeleo chini ya mfumo wa ugatuzi. Lakini inavunja moyo kwamba badala ya kutuongezea, mfumo huu mpya unatupokonya fedha na kuzipeleka katika maeneo ambayo tayari yamepiga hatua kubwa kimaendelea,” Bw Joho akaambia wanachama wa kamati ya seneti kuhusu uhasibu wa pesa za umma (CPAIC).

Chini ya mfumo huo kaunti zinazotoka maeneo kama vile Kaskazini Mashariki, Mashariki na Pwani zitapata mgao wa chini ikilinganishwa na miaka ya nyuma tangu ugatuzi kuanzishwa, ikiwa mfumo huo utapitishwa na Seneti.

Kwa mfano katika eneo la Pwani, endapo mfumo huu utatumiwa katika ugavi wa Sh316.7 bilioni na fedha nyinginezo katika mwaka huu wa kifedha, Mombasa itapoteza jumla ya Sh1.8 bilioni, Kwale (963 milioni), Kilifi (Sh1.5 bilioni), Tana River (Sh205 milioni), Lamu (Sh734 milioni) na Taita Taveta (Sh120 milioni).

Na kaunti ambazo zimepiga hatua kimeandeleo zinatarajiwa kupata sehemu kubwa ya fedha hizo katika mwaka huu wa kifedha wa 2020/2021.

Kwa mfano, Kaunti ya Kiambu itapata Sh1.3 bilioni zaidi ilinganishwa na mgao wake wa Sh9.5 bilioni katika mwaka wa kifedha uliopita wa 2019/2020.

Nayo Nairobi itapokea Sh1.2 bilioni zaidi ya mgao wake wa Sh15.7 bilioni, Uasin Gishu (Sh923 milioni), Nandi (Sh788 milioni), Kajiado (Sh765 milioni), Nakuru (Sh744 milioni), Laikipia (Sh660 milioni), Trans Nzoia (Sh655 milioni), Kirinyaga (Sh538 milioni ), Baringo (Sh537 milioni), Bomet (Sh456 milioni) na Pokot Magharibi (Sh444 milioni).

Kaunti ya Wajir ndio itapoteza fedha nyingi zaidi chini ya mfumo huu mpya kwani mgao wake utapunguzwa kwa kima cha Sh1.9 bilioni.

Na kaunti za Mandera na Marsabit zitapoteza Sh1.8 bilioni kila moja.Kaunti zingine zitakazopoteza ni Wajir (1.9 bilioni) Garissa (Sh1.2 bilion), Mandera (Sh1.8 bilioni), Marsabit (Sh1.8 bilioni), Narok (Sh887 milioni), Isiolo (Sh879 milioni), Turkana (Sh450 milioni), Kitui (Sh219 milioni) na Makueni (Sh302 milioni ).

Wiki jana mfumo huo ulikosa kupitishwa katika seneti baada ya maseneta wagawanyika kwa misingi wana wanapinga na wale wanauunga mkono.

Ilibidi Spika Kenneth Lusaka kuahirisha mjadala huo ili kutoa nafasi kwa pande zote mbili ziweze kuelewana.