Mambo yaenda segemnege
MOHAMED AHMED na FADHILI FREDRICK
USHINDI wa mgombea wa kujitegemea, Bw Feisal Bader katika uchaguzi mdogo wa kiti cha ubunge cha Msambweni, umemuacha kiongozi wa ODM Raila Odinga akiwa amesononeka na kuchanganyikiwa kuhusu kilichosababisha kushindwa kwa mgombea wake.
Hii ni ikizingatiwa kuwa eneo la Msambweni limekuwa ngome ya ODM kwa muda mrefu, jambo lililomfanya Bw Odinga na wakereketwa wake wakiongozwa na Gavana Hassan Joho wa Mombasa kuwa na imani kubwa ya kushinda kiti hicho kwa urahisi.
Hatua ya mrengo wa Rais Uhuru Kenyatta katika Jubilee kuunga mkono mgombeaji wa ODM pia iliimarisha matumaini ya chama hicho kuwa kingeshinda.
Hata hivyo, walipigwa na butwaa jana alfajiri Bw Bader, ambaye aliungwa mkono na Naibu Rais William Ruto, alipoibuka mshindi kwa kura 15,251 dhidi ya Omar Boga wa ODM aliyepata 10,444.
Kulingana na wachanganuzi, ODM wakiongozwa na Bw Odinga walijikaanga wenyewe kwa kuendesha kuingiza masuala ya BBI katika kampeni zao, kutenga wanasiasa wa Kwale, mizozozano baina ya wahusika na kukita kampeni zao mijini.
Kulingana na mchanganuzi wa siasa za Pwani, Profesa Hassan Mwakimako, ODM ilifanya makosa kuendesha kampeni zake katika misingi ya masuala ya kitaifa ikiwemo BBI na handisheki, mambo aliyosema hayakuwa na umuhimu kwa wakazi wa Msambweni.
“Kosa kubwa la kwanza kwa ODM ni kuleta suala la BBI katika kampeni zake na ilikuwa wazi kuwa wakazi wa Msambweni hawakuwa na haja nalo kwa sasa. Ndiposa wapiga kura wengi hawakujitokeza kuwapigia,” akasema Prof Mwakimako.
VIONGOZI KUTOKA NJE YA KWALE
Ripoti zilionyesha kuwa kuhusishwa kwa viongozi kutoka nje ya Kaunti ya Kwale na vita baina ya kikosi cha kampeni za ODM pia kulichangia pakubwa chama hicho kubwagwa.
Katika kura hizo, Bw Bader alishinda katika vituo vingi ikiwemo katika ngome za Bw Boga za Gombato/Bongwe and Ukunda.
Kuhusiana na masuala ya kampeni, upande wa ODM ukingozwa na Gavana Joho ulikita kampeni zake pande za mijini wakati upande wa Bader ulilenga vijijini.
SIASA ZA UBABE
Kampeni za ODM vilevile zilionekana kutowaeleza wakazi faida ya kupigia kura chama chao bali ziliendekeza zaidi siasa za ubabe wa kitaifa hasa kumpiga vita Dkt Ruto.
Uchunguzi wa Taifa Leo ulionyesha kuwa viongozi wa Kwale wa ODM walihisi kutengwa katika kampeni hizo zilizokuwa zinaendeshwa na wanasiasa kutoka nje ya kaunti hiyo.
Siku moja kabla ya uchaguzi, mwanchama wa kikundi cha Ngumu Tupu alipiga simu kwa Taifa Leo na kueleza namna ODM ilivyokuwa inakosea katika kampeni zake kwa kuwaacha wenyeji nje.
“Mgombea wetu hatutambui tena sisi wakazi. Hashiki simu zetu na wala hatuhusishi vilivyo kwenye kampeni. Mikutano mingi imefanyika bila sisi kujua. Pia ameacha wapinzani wetu kufanya mikutano mingi ya kampeni kwa siku zaidi yetu,” akasema mwanachama wa kundi hilo ambaye hakutaka kutajwa.
Malalamishi hayo yalikuwa miongoni mwa ishara za kushindwa kwa ODM, jambo ambalo limepelekea aibu kubwa kwa Bw Odinga, Rais Kenyatta na Bw Joho, ambaye alikuwa anajipiga kifua kama sultani wa siasa za Pwani.
Upande wa Bw Bader uliongozwa na Gavana Salim Mvurya ambaye anaheshimiwa sana katika kaunti hiyo kwa ajenda zake za maendeleo.
GAVANA
“Bw Mvurya pia alitumia nafasi yake kumuhusisha Bw Bader katika kutoa misaada ya masomo kwa wakazi, jambo ambalo watu waliona kuwa Bw Bader tayari anandeleza maendeleo ya mpwa wake Suleiman Dori,” akasema Prof Mwakimako.
Bw Bader alikuwa msaidizi wa Bw Dori na alikuwa anahusika zaidi katika kusimamia pesa za eneo bunge, suala ambalo alitumia kufanyia kampeni zake.
Dkt Ruto alimuunga mkono Bw Bader na kumuezesha kifedha katika kampeni zake.
Jumatano Dkt Ruto alimpa kongole Bw Bader kwa ushindi wake.
“Kongole rafiki yangu Feisal Bader. Ushindi wako unathibitisha imani yetu kwa Mungu na kwa wananchi. Nguvu za demokrasia na za wananchi zimeibuka mshindi,” akasema Dkt Ruto kupitia mtandao wa Twitter.
Mgombea wa ODM Omar Boga jana alikubali kushindwa na akisema kuwa yupo tayari kufanya kazi na Bw Bader.
Alisema kuwa atashikana mkono na mbunge huyo mpya ili kuhakikisha kuwa wakazi wa Msambweni wanahudumiwa ipasavyo.