Habari

Acha katambe

December 5th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na VALENTINE OBARA

WAZIRI Mkuu wa zamani, Bw Raila Odinga, amemtaka Naibu Rais William Ruto ajiandae kupinga mswada wa kura ya maamuzi hadi wakati kura hiyo itakapopigwa.

Akizungumza Ijumaa alipopokea sahihi za wapigakura wanaounga mkono mswada huo chini ya Mpango wa Maridhiano (BBI), Bw Odinga alipuuzilia mbali mapendekezo yaliyotolewa na Dkt Ruto na wandani wake hivi majuzi wakitaka makubaliano ili kusiwe na ushindani kuhusu kura ya maamuzi.

Kinara huyo wa chama cha ODM alitaka pande zote mbili za wanaounga mkono na kupinga ‘ziheshimiane’ na kuwaacha wananchi wajiamulie wanavyotaka debeni, akiahidi kukubali matokeo iwapo BBI itaangushwa kwa kura.

“Hatutaki vitisho wala vita kati ya Wakenya. Acheni debe liwe muamuzi. Mkiwa wengi kutushinda, tutasalimu amri na tukiwashinda pia msalimu amri. Sasa ndiyo mapambano yanaanza,” akasema akiwa Nairobi.

Mbali na Dkt Ruto, kura ya maamuzi imepata pingamizi kutoka kwa mashirika ya kijamii, makundi ya kidini na viongozi kadhaa wa kisiasa. Mnamo Jumatano, Dkt Ruto na wandani wake walitoa masharti kadhaa ambayo walitaka yatimizwe ili waunge mkono marekebisho ya katiba na kuzuia makabiliano ya kisiasa.

Lakini jana, Bw Odinga alisema wapinzani wana nia zao fiche za kibinafsi kwani sababu wanazotoa hazina msingi.

“Wale ambao wako tayari, tutasonga nao mbele. Wakati wa kutoa maoni ulikuwepo, wakaambiwa watoe maoni, wakakataa. Walikuwa wameanza kupinga hata kabla ya mswada kutoka. Sasa wanasema tuongee ili tusiwe na mapambano, tusiwe na mchuano. Mimi kama mwanasiasa sijui popote penye kura ya maamuzi ambapo hakuna pande mbili pinzani,” akasema.

Rais Uhuru Kenyatta ambaye alitarajiwa katika hafla hiyo, hakuhudhuria kwa kuwa alikuwa kwenye mkutano na magavana ambapo aliandamana na Dkt Ruto.

Miongoni mwa mapendekezo ya kikundi cha Tangatanga kinachoongozwa na Naibu Rais yalikuwa kwamba, kura ya maamuzi ifanywe sambamba na Uchaguzi Mkuu wa mwaka wa 2022.

Walidai kuwa hatua hiyo itapunguza gharama ya kuandaa shughuli hiyo ili fedha zitumiwe kwa mambo mengine kama vile kupambana na janga la corona.

Hata hivyo, Bw Odinga alisema Wakenya wana uwezo wa kustahimili hali ilivyo kwani mataifa mengi yameandaa chaguzi kuu licha ya athari za janga la corona.

Aliendelea kusema kuwa wananchi wengi watalemewa uchaguzini iwapo watahitajika kupiga kura ya kurekebisha katiba sambamba na kuchagua viongozi wapya.

“Huo uchaguzi utakuwa na viti sita. Hiyo tayari ni shida kwa wananchi. IEBC (Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka) inataka tuwe tukifanya uchaguzi wa maseneta na magavana wakati tofauti na ule wa wabunge na madiwani, kisha mwingine anasema ongeza tena kura ya saba. Kwa watu ambao hawana elimu ya kutosha huo utakuwa mtihani mgumu,” akaeleza Bw Odinga.

Kuhusu pendekezo la Dkt Ruto kwamba kuwe na maswali kwa kila hoja iliyo katika mswada wa kurekebisha katiba badala ya swali moja linalohitaji jibu la ‘ndiyo’ au ‘la’, Bw Odinga alisema mwelekeo huo utafanya wananchi kuchanganyikiwa hasa wasiojua kusoma.

Hayo yaliungwa mkono na Seneta wa Siaya, Bw James Orengo.

“Katiba inahitaji tupigie kura mswada, si maswali. Tutapigia kura mswada,” akasema Kiongozi huyo wa Wachache katika Seneti.

Kufikia Ijumaa, waratibu wa ukusanyaji sahihi za BBI walisema zilikuwa takriban milioni tano, huku wakitarajia kuzifikisha hadi milioni sita.

Mbunge wa Suna Mashariki, Bw Junet Mohammed ambaye ni mmoja wa waratibu alikanusha kwamba machifu walitumiwa kukusanya sahihi za wananchi kwa lazima. Alidai machifu hao walikuwa wanatoa tu ulinzi kwa makundi yaliyopewa kazi ya kukusanya sahihi.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Kike wa Kiambu, Bi Gathoni Wamuchomba alipinga msimamo wa Dkt Ruto kwamba wanawake hawajatendewa haki katika mapendekezo yaliyo kwenye mswada wa kurekebisha katiba.

“Wanaume achaneni na wanawake waongelee masuala ya wanawake. Mahali ambapo tumewapa nafasi mtushughulikie mnatushughulikia vizuri na hatujateta. Hayo mengine ya siasa na uongozi tuachieni tujitetee,” akasema.

Kauli hii iliungwa mkono na Kiongozi wa Wengi bungeni, Bw Amos Kimunya, aliyetaka wanawake wajihadhari wasipotoshwe.

“Wanadanganya wanawake waende mikutano yao ya hadhara kutingisha viuno lakini wasiwe bungeni. Ni heri mswada mzima uanguke lakini wanawake waongezwe uongozini,” akasema.

Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa, Bw John Mbadi, alisema wanatarajia IEBC itachukua wiki moja pekee kuthibitisha sahihi za wapigakura zilizokusanywa ili mchakato mzima usicheleweshwe.