Afisa aliyehepa baada ya mauaji ya wakili kukaa rumande siku 14
AFISA wa Polisi Kenneth Kipkemboi Sang amezuiliwa kwa siku 14 ili kuhojiwa kuhusu mauaji ya wakili Mathew Kyalo Mbobu na mtaalamu wa tiba ya ubongo, Dkt Victoria Nthunya Mutiso.
Sang, aliyekamatwa Oktoba 24, 2026, jijini Eldoret alipokuwa akijaribu kuuza gari lake, alifikishwa mbele ya Hakimu Mkuu Paul Mutai katika Mahakama ya Milimani, Nairobi.
Upande wa mashtaka ulisema bastola aliyokabidhiwa afisa huyo ndiyo iliyotumika kumuua Dkt Mutiso Julai 29, 2026. Pia alituhumiwa kutoroka kazi na kukimbilia nje ya nchi baada ya mauaji hayo.
Mwendesha mashtaka Virginia Kariuki aliomba mshukiwa azuiliwe bila dhamana, akisema anaweza kutoroka au kuathiri mashahidi. Sang alipinga ombi hilo, akisema uchunguzi tayari umefanyika kwa kina.
Hakimu Mutai aliamuru azuiliwe katika Kituo cha Polisi cha Kilimani hadi Novemba 9, 2026, uchunguzi ukiendelea kubaini nafasi yake katika mauaji hayo.