HabariHabari za KauntiHabari za Kitaifa

Majonzi mtaa ukifiwa na mapasta watatu kupitia ajali Mtito Andei

Na WINNIE ATIENO October 27th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

WAKAZI wa mtaa wa Bangladesh, eneo la Mikindani, Mombasa, wamezama katika majonzi kutokana na vifo vya wachungaji watatu na waumini wengine katika ajali iliyoangamiza watu 24 katika eneo la Kanga, barabara ya Mombasa-Nairobi, Kaunti ya Makueni, Jumapili asubuhi.

Wachungaji Joseph Vura wa Campaign for Salvation and Healing Ministry (CASHEM), Fonex Paul wa River of Life na Isaac Juma wa Grace Healing Sanctuary walikuwa kati ya waliokuwa wakirejea kutoka mazishi ya mwenzao katika Kaunti ya Kakamega, basi walimokuwa lilipogonga lori la mizigo lililokuwa limesimama.

Katika mtaa wa Bangladesh, familia na marafiki wa marehemu bado wanatatizika kukubali ukweli wa vifo hivyo, huku wengine wakipanga mazishi na kuomboleza wapendwa wao.

Bi Judith Awino, ambaye aliishi na shemeji yake Hollon Oduor Waganda kwa miaka 10, alisema alipokea habari za ajali hiyo alipokuwa akiomba katika Kanisa la Lamb of God, Mikindani.

“Mume wangu alinipigia simu kuniuliza kuhusu wachungaji waliofariki katika ajali. Hakujua kwamba mdogo wake pia alikuwa ndani ya basi hilo. Tulipojaribu kumpigia simu, hakupokea,” alisema.

Familia ilimtuma ndugu mwingine wa marehemu aliyekuwa Samburu, kaunti jirani ya Kwale, kwenda Makueni kuthibitisha hali yake. Baadaye aliwapigia simu na kuwathibitishia habari walizokuwa wakihofia.

Bi Awino alisema Waganda alikuwa ametembelea nyumbani kwake Jumanne kuazima sanduku la kusafiria.

“Waliondoka, lakini sasa wanarejea nyumbani wakiwa wamefariki. Familia yetu imeshtuka,” alisema.

Mwili wa Waganda ulikuwa ukisubiri kuhamishwa hadi hifadhi ya ya Hospitali ya Coast General kabla ya kusafirishwa Siaya kwa mazishi.

Katika Mataa ya Ndege, Jomvu, wakazi wanaomboleza Mchungaji Fonex Paul, aliyehudumu katika kanisa lake kwa zaidi ya miaka 10. Jirani yake Peter Bendi alisema marehemu alikuwa mwenye huruma, mchangamfu na aliyesaidia watoto wa eneo hilo kwa masomo ya ziada.

Mchungaji huyo ameacha mkewe Ann Biyaki.

Katika Grace Healing Sanctuary, mchungaji msaidizi Fredrick Ochieng Odhiambo alisema kifo cha Juma kimeacha pengo kubwa katika jamii.

Juma ameacha mke na watoto wanne.

Marehemu Vura, Juma na Fonex walikuwa na makanisa yaliyokuwa umbali mfupi katika mtaa huo wenye wakazi wengi.

Wakati huo huo, Gavana wa Mombasa Abdulswamad Nassir na Mbunge wa Likoni Mishi Mboko Jumatatu walitembelea maaskofu Zachariah Mwagandi na Cosmas Oduor Nyangweso, wanaopokea matibabu katika Hospitali ya Coast General baada ya kunusurika ajali hiyo.

Ajali hiyo ilitokea takriban wiki tatu baada ya watu 17 waliokuwa wakisafiri kwenda Subukia Shrine kufariki katika ajali ya Salama, barabara hiyo hiyo, Oktoba 4