Afisa wa polisi mbaroni kwa kushambulia wenzake wawili kituoni
MAAFISA wa upelelezi Kitengela, Kaunti ya Kajiado, wamemkamata afisa wa polisi aliyewashambulia na kuwajeruhi wenzake wakiwa kituoni.
Kulingana na ripoti ya polisi iliyosajiliwa katika Kitabu cha Matukio (OB) nambari 27/22/05/2025, konstebo huyo wa polisi kutoka kituo cha polisi cha Athi River katika Kaunti ya Machakos alikamatwa na maafisa wa trafiki kwenye barabara ya Nairobi–Namanga kwa makosa ya trafiki lakini akawa mkali.
Afisa huyo, aliyekuwa mlevi wakati wa tukio, alishtakiwa kwa kuendesha gari lisilo na bima, kuendesha akiwa amelewa, kukaidi maagizo ya mdomo ya afisa wa trafiki, na kukataa kukamatwa.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa alipofikishwa katika kituo cha polisi cha Kitengela na kufanyiwa ukaguzi kabla ya kuwekwa seli, mshukiwa aliwashambulia maafisa wawili waliokuwa kazini; mmoja akiwa mlinzi wa seli na mwingine mlinzi wa kituo.
Afisa mmoja alijeruhiwa kichwani na kwenye mguu wa kushoto, huku mwenzake akivunjika kidole kidogo cha mkono wa kulia kabla ya wote wawili kukimbizwa hospitalini.
Maafisa waliojeruhiwa walipokea fomu za P3 kujiandaa kufungua mashtaka ya kushambuliwa.
Mshukiwa anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Kitengela akisubiri hatua zaidi za polisi. Gari alilokuwa akiendesha pia limezuiliwa katika kituo hicho.
Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Isinya Patrick Manyasi, aliambia Taifa Leo kuwa afisa huyo atachukuliwa hatua za kinidhamu ndani ya Huduma ya Polisi.
“Sheria itafuata mkondo wake. Huduma ya Polisi haina nafasi kwa maafisa wanaopotoka,” alisema Bw Manyasi.