Habari

Afrika yakosolewa kwa kushindwa kuzuia mikasa

December 10th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na JUMA NAMLOLA

MJUMBE Maalum wa Umoja wa Ulaya, Bi Jutta Urpilainen, ameyahimiza mataifa wanachama wa Muungano wa Afrika, Carribean na Pacific (ACP) yakabili majanga kabla hayajatokea.

Akihutubu wakati wa ufunguzi wa kongamano la viongozi wa mataifa hayo jijini Nairobi Jumanne, Bi Urpilainen alisemam mikasa mingi inayotokea ulimwenguni huchukuliwa kuwa majanga kwa kuwa watu huwa hawajajipanga.

“Kwa mfano hapa Kenya majuzi, maporomoko ya ardhi na mvua zilisababisha vifo vya zaidi ya watu 120. Maporomoko yanaweza kuzuiwa kupitia utunzaji mazingira,” akasema.

Mwanasiasa huyo wa Finland alieleza jinsi ambavyo kutokana na uzembe au ulafi, watu wengi wamekufa na wengine kuwa hatarini, kwa kuwepo shughuli haramu zinazochangia kubadilika kwa hali ya hewa.

“Umoja wa Ulaya unatuma rambirambi zake kutokana na vifo hivi. Lakini nasikitika kuwa pole pekee haipozi. Haifai kuwa tunaketi tu na kusubiri majanga yatokee kisha tuwape pole waathiriwa. Yatupasa tushughulike sasa na kukabili athari za mazingira,” akasema.

Rais wa Ghana, Nana-Akufo Addo akichangia suala la mazingira, alionya kuwa huenda mataifa wanachama yasipate ufanisi wowote wa kiuchumi na maendeleo iwapo hawataanza sasa kupanga mikakati ya kukabili majanga.

‘Kwenye mipango yetu ya maendeleo, tuna mambo mengi ambayo tungependa kuyatimiza. Haya yatawezekana tu ikiwa kama wanachama wa ACP, tutaanza mikakati ya kukabili mabadiliko kwa mambo yamekuwa chanzo cha maafa kote ulimwenguni,” akasema.

Kwenye ufunguzi wa kongamano hilo, Rais Uhuru Kenyatta alipokezwa urais wa ACP kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo.

Rais Kenyatta aliahidi kuwa chini ya uongozi wake, atahakikisha mataifa wanachama yanafanikiwa kutimiza malengo makuu kuhusiana na uchumi.Kongamano hilo linakamilika leo.