Habari

AFYA: Ruto amsuta Raila

December 9th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

NAIBU Rais William Ruto amemshutumu aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga kwa kudunisha matakwa ya wahudumu wa afya walioko mstari wa mbele katika vita dhidi ya janga la Covid-19 nchini.

Akiongea katika Kaunti ya Kericho Dkt Ruto alisema Jumanne hatua ya Bw Odinga kuweka kando masuala yanayowaathiri wahudumu wa afya wakati huu wa janga lililoathiri uchumi na kusababisha vifo inaonyesha kuwa yeye (Odinga) ni kiongozi asiyewajibika.

“Haina maana mtu kusema masuala ya kisiasa kama vile marekebisho ya katiba kupitia mswada wa BBI yanapaswa kushughulikiwa kwanza kabla ya malalamishi yaliyoibuliwa na wahudumu wa afya ilhali wao ndio wanajeshi wetu katika vita dhidi ya janga la corona,” akasema Dkt Ruto.

Alikuwa akiongea katika Kericho Golf Club wakati wa ibada ya mazishi ya Kanali Jenerali (Mstaafu) John Koech aliyefariki majuzi.

Dkt Ruto aliwataka viongozi kulipa kipaumbele suala hili la janga la Covid-19 ambalo limevuruga uchumi badala ya masuala mengine kama vile mchakato wa kura ya maamuzi kupitia mswada wa BBI.

Mnamo Jumatatu Bw Odinga aliwataka wahudumu wa afya wanaogoma kuweka kandao matakwa yao wakati huu ambapo Kenya inakabiliwa na changamoto ya kiuchumi iliyosababishwa na janga la corona.

Akiongea mjini Kisumu, Bw Odinga aliwataka wahudumu hao kuendelea kushiriki mazungumzo na serikali kuu na zile za kaunti ili kupata muafaka kuhusu matakwa yao badala ya kugoma.

“Mgomo utasababisha hali ya sasa kuwa mbaya zaidi. Hii ni kwa sababu sio wahudumu wa afya pekee walioathirika na janga hili bali wananchi kwa ujumla,” akasema.

Lakini Jumanne Dkt Ruto akamjibu kwa kusema: “Tunafaa kulenga kuwapa wahudumu wa afya vifaa-kinga (PPE) na tuwalipe mishahara na marupurupu hitajika. Serikali za kaunti zinastahili kuyapa kipaumbele masuala yaliyoibuliwa na madaktari, wauguzi, maafisa wa kliniki na vitengo vingine vya wahudumu wa afya ambao wako katika mstari wa mbele katika vita dhidi ya janga la corona.”

Naibu Rais alisema serikali kuu imeagiza wizara ya afya kushirikiana na viongozi wa vyama vya kutetea masilahi ya wahudumu wa afya kusuluhisha masuala yaliyoibuliwa na wanachama wao.

“Ikiwa taasisi zetu za afya zilikuwa zikifanya kazi vizuri, kuna uwezekano mkubwa kwamba Jenerali Koech hangefariki. Kama viongozi twapaswa kuchukulia masuala ya afya kwa uzito,” Dkt Ruto akasema.

Viongozi wa kisiasa walioandamana na Naibu Rais pia walimshambulia Bw Odinga kwa kuendeleza kampeni za marekebisho ya Katiba wakati kama huu ambapo janga la Covid-19 ni kero kwa taifa.

Miongoni mwa wanasiasa hao walikuwa Gavana wa Kericho Paul Chepkwony, naibu wake, Susan Kikwai, maseneta; Kipchumba Murkomen (Elgeyo Marakwet ); Millicent Omanga (Seneta Maalum); Aaron Cheruiyot (Kericho ); Florence Bore (Mbunge Mwakilishi wa Wanawake Kericho ); Nelson Koech (Mbunge wa Belgut); Johana Ngeno (Mbunge wa Emurrua Dikirr), Silvanus Maritim (Mbunge wa Ainamoi) na Katibu Mkuu wa Kanu Nick Salat.