Aibu wakazi wakienda haja eneo wazi katikati ya mji wa Murang’a
KATIKA mji wa Murang’a kuna eneo lililogeuka kuwa uwanja wa wazi wa kwenda haja, lililo nyuma ya Benki ya Kenya Commercial Bank (KCB), katikati ya majengo ya kibiashara na nyumba za kupanga.
Eneo hilo lilianza kutumiwa na watu kwenda haja baada ya choo cha umma kilichokuwapo kuvamiwa na kuharibiwa, kisha kikakosa kukarabatiwa, hali iliyowalazimu wakazi na wageni kutumia eneo la wazi lililo karibu.
Wakazi walikuwa wakifika na kukuta choo kimeharibiwa na kikiwa kichafu na wakaanza kutumia eneo hilo, na baada ya muda, sehemu hiyo imegeuka kuwa aibu inayoshuhudiwa leo.
Hali imekuwa mbaya zaidi kutokana na baadhi ya wapangaji kutumia eneo hilo kutupa takataka.
“Kinachokera zaidi ni watu kwenda haja juu ya takataka hizo kisha kuzichoma moto. Harufu ya kinyesi cha binadamu kinachoungua na taka hufanya maisha ya wapangaji wa karibu kuwa mateso,” alisema Bi Eunice Waithera, mpangaji katika eneo hilo.
Cha kushangaza ni kuwa hali hii inajitokeza huku Gavana wa Murang’a, Dkt Irungu Kang’ata, akiendeleza mradi wake wa mji wa kisasa, uliotuzwa majuzi.
Dkt Kang’ata alisifiwa kwa kile kilichoelezwa kama “mbinu bunifu ya kubadilisha miji mikuu ya Kaunti ya Murang’a kwa kuboresha miundombinu, ikiwemo kuweka lami barabarani, taa za barabarani, na kuboresha mifumo ya maji taka na usafi ili kuchochea biashara na usalama.”
Mpango wake wa Smart City ulitambuliwa katika Tuzo za Smart Cities Forum 2025 zilizofanyika katika Kituo cha Biashara cha Two Rivers, Nairobi.
“Murang’a ni mji wa aina gani ya kisasa ikiwa una aibu kama hii, ambako majitaka hukauka juani au husombwa na mvua na kuingia katika makazi kuelekea kwenye vyanzo vya maji?” alihoji Bw James Kimani, 83, mkazi wa eneo hilo.
Ni jambo la kawaida sasa kuona wanaume na wanawake wakielekea eneo hilo kwa haja kubwa au ndogo, huku wakazi wakilalamikia ukimya wa mamlaka husika.
“Tufanye nini? Tumelalamika mara nyingi kwa serikali ya kitaifa na ya kaunti. Hata tumejaribu kutumia ulinzi wa jamii kushughulikia tatizo hili, lakini hakuna kilichofaulu,” alisema Bw Stephen Mwangi, mfanyabiashara karibu na eneo hilo.
Afisa Mkuu wa Afya wa Kaunti ya Murang’a, Bw Eliud Maina, alihusisha uhaba wa vyoo vya umma na miaka ya kutelekezwa pamoja na unyakuzi wa ardhi.
Bw Maina aliambia Taifa Dijitali kuwa serikali ya kaunti inafahamu hali hiyo ya aibu na iko katika mchakato wa kutenga bajeti ili kufunga eneo hilo na kujenga choo cha umma kinachotunzwa ipasavyo katika eneo hilo.
Harufu kali, panya na nzi sasa ndizo zinatawala eneo hilo lenye ukubwa wa takribani futi 100 kwa 10, ambalo limefunikwa na kinyesi cha binadamu kinachoongezeka kila siku.
Katika hali mbaya zaidi, wanawake wako katika hatari ya kushambuliwa wanapolazimika kutumia eneo hilo kwenda haja.
Bw David Kuria, mwanachama wa mpango wa usalama wa Nyumba Kumi, alisema eneo hilo ni hatari kubwa kiusalama.
“Tunapokea takribani ripoti tatu kila wiki za watu kuporwa katika eneo hilo,” alisema.
Zaidi ya hayo, maafisa fisadi wa kaunti na polisi wachache wasio waaminifu wanaripotiwa kutumia hali hiyo kuwanasa watu na kudai hongo.Ingawa wanawake ndio wanaoathirika zaidi, wanaume na watoto pia ni wahanga.
“Hivi majuzi nilibanwa na haja ndogo. Niliuliza ni wapi ningepata choo cha umma nikaambiwa kilicho karibu kiko mbali. Fundi wa viatu alinielekeza nyuma ya maduka fulani. Afisa wa polisi aliyevalia sare alinivamia na nililazimika kutoa Sh300. Hiyo ni bei kubwa sana kwa kukojoa,” alisema Bw Martin Mutiso, aliyekuwa ametoka Hospitali ya Rufaa ya Murang’a kumtembelea jamaa mgonjwa.Shinikizo sasa linaongezeka kwa serikali ya kaunti kushughulikia kile wakazi wanachokitaja kama bomu la kiafya linalosubiri kulipuka.
“Tunaomba serikali ya kaunti ituokoe haraka. Hali hii inadhalilisha sana utu wa binadamu. Murang’a, makao makuu ya kaunti, haina vyoo vya umma vya kutosha vinavyopatikana kwa urahisi, hasa kwa wageni,” alisema Bi Jacinta Mugure, ambaye amefanya biashara mjini humo kwa miaka 20.
Aliongeza kuwa mji una vyoo viwili pekee vya umma vinavyofanya kazi, navyo viko maeneo ya pembezoni.
“Kimoja kiko katika eneo hatari la Kayole ambako magenge ya dawa za kulevya yanapatikana,” alisema.
Choo kingine kiko karibu na kituo kidogo cha Mukurwe-ini, ambako watumiaji hutozwa kati ya Sh10 na Sh20.
Afisa Mkuu wa Afya wa Kaunti ya Murang’a, Bw Eliud Maina, alihusisha uhaba wa vyoo vya umma na miaka ya kutelekezwa pamoja na unyakuzi wa ardhi.
Aliongeza kuwa baa nyingi mjini humo hazina vyoo vinavyofaa, hali inayowalazimu wateja kutumia maeneo ya wazi.
“Tulikuwa na choo cha umma karibu na soko la Murang’a Marikiti, lakini kimegeuzwa kuwa maduka ya biashara,” alisema.
Bw Maina aliambia Taifa Dijitali kuwa serikali ya kaunti inafahamu hali hiyo ya aibu na iko katika mchakato wa kutenga bajeti ili kufunga eneo hilo na kujenga choo cha umma kinachotunzwa ipasavyo katika eneo hilo.