Aisha Jumwa aachiliwa kwa dhamana ya Sh4 milioni pesa taslimu
Na BRIAN OCHARO
MBUNGE wa Malindi, Bi Aisha Jumwa aliyezuiliwa korokoroni kwa siku ya nne Alhamisi, ameachiliwa Ijumaa kwa dhamana ya Sh4 milioni pesa taslimu na mahakama ya Mombasa.
Alhamisi jioni, Bi Jumwa na mlinzi wake Geoffrey Otieno walirejeshwa katika seli ya kituo cha polisi cha Bandarini ambako wamekuwa tangu Jumatatu, baada ya kukanusha mashtaka ya mauaji.
Mbunge huyo wa chama cha ODM ambaye kwa sasa anaegemea mrengo wa siasa wa Naibu Rais William Ruto, alikanusha kuhusika na mauaji ya mfuasi wa chama cha ODM, Bw Jola Ngumbao, wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa wadi ya Ganda, Kaunti ya Kiifi.
Jaji wa Mahakama Kuu, Njoki Mwangi ambaye anasikiza kesi hiyo ya mauaji ametoa uamuzi baada ya kusoma stakabadhi zote.
Stakabadhi hizo zilitumwa na waendesha mashtaka na mawakili wa Bi Jumwa ambao waliomba aachiliwe kwa dhamana.
Wawili hao wameshtakiwa kwamba, mnamo Oktoba 15, 2019 walimuua Bw Jola Ngumbao.
Jana Alhamisi washukiwa walifikishwa mahakamani saa tatu asubuhi tayari kujibu mashtaka lakini shughuli za mahakama zikasitishwa kwa muda kuruhusu waendesha mashtaka kujiandaa.
Ripoti ya ukaguzi wa hali ya kiakili ya Bw Otieno haingeweza kupatikana miongoni mwa stakabadhi ambazo waendesha mashtaka walikuwa wamewasilisha mahakamani.
Isitoshe, Jaji Mwangi alihoji uhalali wa ripoti ya hali ya afya ya Bi Jumwa, ambayo ilikuwa na sahihi isiyofanana na ile ya mtaalam ambaye alimfanyia mbunge huyo ukaguzi katika Hospitali Kuu ya Pwani.
Vile vile, imeibuka kuwa serikali iliwaondoa walinzi wa Bi Jumwa baada yake kutangaza waziwazi kwamba anaunga mkono azma ya Naibu Rais William Ruto ya kuingia Ikulu 2022.
Wakili Danstan Omari aliambia mahakama kwamba, Bi Jumwa alilazimika kukodi walinzi wa kibinafsi kumlinda.
“Kwa sababu ya muegemeo wake wa kisiasa, serikali ilimpokonya walinzi. Ameamua kutumia fedha zake kukodi huduma za walinzi wa kibinafsi,” akasema Bw Omari.
Huku Afisi wa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) ikiomba mahakama isimwachilie huru mbunge huyo kwa dhamana, mawakili wake waliwasilisha ombi wakitaka aachiliwe kwa dhamana ili aendelee na majukumu yake kama mbunge kesi inapoendelea.
DPP Noordin Haji aliwakilishwa na Jami Yamina na Alloys Kemo ambao wanataka washukiwa waendelee kuzuiliwa kwa sababu huenda wakavuruga mashahidi ambao hawajafika mahakamani kusema yaliyojiri siku ambayo Ngumbao alipigwa risasi na kuuawa.
Jumwa na Bw Otieno waliripotiwa kuvamia nyumbani kwa diwani wa Wadi ya Ganda, Reuben Katana na wakasababisha vurugu.
Waendesha mashtaka wanasema kuwa wawili hao ni watu wenye ushawishi mkubwa na wanaweze kuingilia mashahidi na hivyo kuvuruga kesi hiyo, ambayo iko katika siku zake za mwanzo.
“Ni kawaida kwamba wanaokabiliwa na makosa kama hayo wanaweza kuwafikia mashahidi wa upande wa mashtaka. Tunaamini kuwa hii ni sababu yenye uzito kuwanyima dhamana washukiwa,” akasema Bw Kemo.