Habari

Al-Shabaab watatu wauawa Kiunga

July 15th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA KALUME KAZUNGU

MAGAIDI watatu wa Al-Shabaab waliuawa huku polisi wawili wakijeruhiwa vibaya pale kilipuzi cha kutegwa ardhini kilipolipuka kwenye eneo la Kiunga kuelekea mpakani mwa Kenya na Somalia Jumatatu.

Kilipuzi hicho kinashukiwa kuzikwa barabarani na magaidi hao. Walinda usalama waliozungumza na Taifa Leo Dijitali kutoka eneo la tukio na kuomba kutotajwa walisema shambulizi hilo lilitokea majira ya saa tatu unusu asubuhi.

Kulingana nao, magaidi wa Al-Shabaab walianza kuwafyatulia maafisa wa usalama wa kitengo cha polisi wa kulinda mipaka (RBPU) risasi baada ya gari lao kukanyaga kilipuzi hicho na kulipuka.

Maafisa wa usalama walijibu kwa kuwamiminia risasi magaidi hao wanaodaiwa kujificha kwenye kichaka kando ya barabara karibu na eneo ambapo walikuwa wametega kilipuzi.

“Kulikuwa na shambulizi lililotokea eneo la Kiunga karibu na mpaka wa Lamu na Somalia. Magaidi wa Al-Shabaab walitega kilipuzi kuwalenga maafisa wetu waliokuwa wakishika doria eneo hilo.

“Gari walimokuwa wakisafiria maafisa wetu lilikanyaga kilipuzi ambacho kililipuka baadaye. Magaidi walianza kuwamiminia risasi maafisa wetu, ambapo makabiliano makali yalizuka. Ni wakati huo ambapo magaidi watatu wa Al-Shabaab waliuawa ilhali maafisa wetu wawili wa polisi wa kitengo cha RBPU wakijeruhiwa vibaya,” akasema afisa huyo kwa njia ya simu.

Magaidi watatu waliuawa ilhali polisi wawili wakijeruhiwa kwenye shambulizi eneo la Kiunga karibu na mpaka wa Kenya na Somalia. Picha/ Kalume Kazungu

Maafisa wa utawala waliozungumza na Taifa Leo pia walithibitisha tukio hilo la uvamizi.

Naibu Kamishna wa Kaunti Ndogo ya Lamu Mashariki, David Lusava alikiri kupokea taarifa kuhusu shambulizi hilo lakini akasema bado anasubiri habari zaidi kuhusiana na tukio hilo.

“Nimepokea habari kwamba kuna shambulizi lililotekelezwa na Al-Shabaab eneo la Kiunga lakini sijajua ni mahali gani hasa shambulizi hilo limetekelezwa. Bado ninasubiri taarifa zaidi kutoka eneo la tukio. Kwa sasa sijui ni nani ameuawa wala kujeruhiwa,” akasema Bw Lusava.

Kiunga, Ishakani na maeneo yote ya mpakani mwa Lamu na Somalia yako chini ya maafisa wa usalama wanaotekeleza operesheni ya Linda Boni.

Mnamo Septemba, 2015, serikali ya kitaifa ilizindua Operesheni ya Linda Boni, lengo kuu likiwa ni kuwafurusha magaidi wa Al-Shabaab wanaoaminika kujificha ndani yam situ wa Boni.

Shambulizi la Jumatatu linajiri mwezi mmoja baada ya magaidi wanne wa Al-Shabaab kufariki na wengine kujeruhiwa pale kiliopuzi walichojaribu kutega barabarani kilipolipuka ghafla kabla ya muda wake.