Aladwa, Arati waashiria Sakaja atakula hu ODM
ODM Alhamisi ilitangaza kuwa itawasilisha mgombeaji wa kiti cha ugavana 2027 huku ikishikilia tikiti itapewa tu mwanachama wa chama hicho.
Tangazo hilo sasa ni pigo kwa Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja ambaye alionekana kuwa pazuri kutwaa tikiti ya ODM kutokana na ukuruba aliokuwa nao na marehemu Kiongozi wa chama Raila Odinga.
Bw Odinga miezi miwili iliyopita aliwarai madiwani wa ODM wasitishe mpango wa kumbandua Bw Sakaja madarakani na pia alifasiriwa kama amemuidhinisha wakati wa hafla ya maombi Ukumbi wa Bomas. Maombi hayo yalikuwa ya kumwombea Raila kwenye safari yake ya kuwania uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).
Ukuruba wa Raila/Sakaja ulionekana kuwatetemesha wabunge Babu Owino (Embakasi Mashariki) na Tim Wanyonyi (Westlands) ambao hapo awali walionekana wangetumia ODM kuwahi ugavana.
Bw Owino alianza kujihusisha na mrengo wa upinzani huku Bw Wanyonyi akihamisha siasa zake hadi Kaunti ya Bungoma ambako analenga kiti hicho hicho.
Alhamisi wanachama wa ODM Kaunti ya Nairobi walisema kuwa ni mwanachama kindakindaki ndiyo atapeperusha bendera ya chama hicho.
Katika mkutano huo ulioongozwa na Naibu Kiongozi wa chama Simba Arati, Mbunge wa Makadara George Aladwa alitangaza kuwa atatumia ODM kuwania ugavana 2027.
“Nataka niwaambie kuwa ukitaka kuwa gavana Nairobi, lazima uwe mwanachama wa ODM, ukitaka kuwa seneta Nairobi lazima pia uwe na ODM,” akasema Bw Arati.

Bw Sakaja alishinda 2022 na UDA na bado ni mwanachama hadi leo.
Bw Aladwa naye alisema chama kitaanza shughuli mbalimbali kuimarisha uungwaji mkono wake jijini, ikiwemo kumpigia debe mwaniaji wake katika uchaguzi mdogo wa wadi ya Kariobangi North Michael Majua.
“Mtu asifikirie kuwa wanachama wa ODM watamuunga mkono 2027 kama bado wapo vyama vingine. Natangaza kuwa nitawania ugavana 2027, nitashinda na tukutane debeni,” akasema Bw Aladwa.
Iwapo Bw Owino atahiari kutumia ODM kuwania ugavana basi itabidi wawili hao washiriki mchujo na mshindi awahi tiketi.
Mabw Arati na Aladwa walikuwa wameongoza mkutano wa wanachama wa ODM Kaunti ya Nairobi.