HabariSiasa

Alice Wahome amshtaki Matiang'i

February 13th, 2020 1 min read

Na MAUREEN KAKAH

MBUNGE wa Kandara Alice Wahome, amewashtaki waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i na Inspekta Jenerali wa polisi Hillary Mutyambai kwa kumpokonya walinzi.

Kwenye kesi aliyowasilisha katika Mahakama Kuu, mbunge huyo anadai hajawahi kushtakiwa kwa makosa yoyote ya uhalifu ilhali walinzi wake waliondolewa kufuatia amri ya Bw Mutyambai.

Kwenye agizo alilotoa Januari 20, Bw Mutyambai alisema viongozi wanaokabiliwa na mashtaka ya uhalifu watapokonywa walinzi wa serikali.

Bi Wahome alidai amekuwa akilindwa na maafisa wa usalama kwa miaka saba tangu 2013 alipochaguliwa kuwa mbunge, na kuwa kumpokonya walinzi kunahatarisha maisha yake.

Walinzi katika boma lake waliondolewa Septemba mwaka jana na walinzi wake binafsi wakaondolewa mapema mwezi huu.

Awali, alikuwa amelalamika kuwa hakupatiwa sababu za kuondolewa kwa walinzi hao.