Alivyojikaanga
BENSON MATHEKA na PETER MBURU
NAIBU RAIS William Ruto alijifungulia mlango wa masaibu yanayomkabili kisiasa kwa sasa, kutokana na mazoea yake ya kumkaidi mkubwa wake Rais Uhuru Kenyatta, kujaribu kuvamia ngome yake ya Mlima Kenya na kudhibiti chama cha Jubilee.
Hii ilimfanya Rais Kenyatta kukereka na kuchukua hatua asionekane kuwa kiongozi asiye na makali huku umaarufu wa Dkt Ruto ukiongezeka.
Wadadisi wasema kwamba, Dkt Ruto alilewa na mamlaka akapuuza wanasiasa waliomshauri kutuliza boli hadi akajitumbukiza katika hali ya sasa ya kutengwa serikalini.
Wakati mmoja, Katibu Mkuu wa Muungano wa vyama vya wafanyakazi nchini, Francis Atwoli alimweleza Ruto “kuenda chini ya maji” kwa muda na kumheshimu Rais.
Baadaye, Bw Atwoli alisema Rais Kenyatta alifanya makosa kuungana na Dkt Ruto.
Dkt Ruto kwa wakati huu, anakabiliwa na masaibu ambayo wengi wanasema alijitafutia mwenyewe kwa kulenga kumpiku mkubwa wake kwa umaarufu na ushawishi.
Kuanzia 2018 baada ya Rais Kenyatta na Dkt Ruto kuchaguliwa kuhudumu muhula wao wa pili, Dkt Ruto alikuwa akifanya kinyume na matakwa na amri za Rais makusudi kuthibitisha alikuwa akifanya maamuzi serikalini.
Licha ya Rais Kenyatta kuwakanya viongozi kuendesha siasa za mapema, Dkt Ruto amekuwa akiwaongoza wafuasi wake kuzunguka nchini, wakimtawaza kama mgombea urais wa pekee wa chama cha Jubilee kwenye uchaguzi Mkuu wa 2022.
Wadadisi wanasema, Naibu Rais alianza kampeni ya kuteka nyara ngome ya Rais ya Mlima Kenya, kwa kuzuru kaunti za eneo hilo mara kwa mara, akiandamana na viongozi wa eneo ambao wamekuwa wakimkashifu Rais kwa kupuuza wakazi kimaendeleo.
Ili kuzima ziara hizo, Rais Kenyatta alimteua Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiangi kushirikisha miradi ya maendeleo ya serikali. Ruto alipuuza uteuzi huo.
Katika mchujo wa chama cha Jubilee, kabla ya uchaguzi mkuu wa 2017, Dkt Ruto alihakikisha ni wandani wake kutoka Mlima Kenya waliopata tiketi na kuwatema washirika wa Rais.
Ziara zake eneo hilo zilizidi na tetesi zikaibuka kuwa Rais alikuwa akipoteza umaarufu nyumbani kwake, na watetezi wake kuanza kulemewa kukabili wafuasi wa Dkt Ruto.
Wakati fulani mwaka uliopita, Rais alionekana mwenye hasira alipowatahadharisha viongozi wa Mlima Kenya ambao alisema kazi yao ni kupiga siasa kila mara badala ya kufanya kazi, kuwa chuma chao kilikuwa motoni.
“Hawa wanasiasa tulichagua wasidhani mimi ni mvulana wao, na hawatanizuia kusonga kwa ile njia ninayotengenezea watu wetu. Wasidhani huwa wananitisha, nikiamua sitaki siasa, nitawatoa kote wanakoenda,” Rais akasema, katika hafla ambayo naibu wake alikuwapo.
Lakini licha ya tofauti za kisiasa, Naibu Rais pia alionekana kumkaidi Rais alipotangaza vita dhidi ya ufisadi 2018.
Baada ya maafisa kadhaa kukamatwa, Dkt Ruto na wafuasi wake walianza kulalamika kuwa vita hivyo vilikuwa vikiendeshwa kisiasa, na kukashifu Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) kuwa ilikuwa ikitumiwa na “wakora”.
“Hatutakubali watu wakora waende watumie afisi ya DCI kuendesha porojo na propaganda zinazolenga kuhujumu miradi ya serikali, (miradi) ya mabwawa na mingine kwa lengo la kisiasa,” Dkt Ruto akasema mnamo Machi mwaka jana.
Hii ni licha ya Rais kusisitiza kuwa alikuwa na imani na DCI na DPP.
Vilevile, Dkt Ruto amekuwa mmoja wa wapinzani wakuu wa Jopo la Maridhiano (BBI), ambalo amekuwa akililaumu kuwa linapanga kufanyia katiba marekebisho, bila kuhusisha wananchi.
Hii ni licha ya kuwa, Rais Kenyatta ni mtetezi mkuu wa jopo hilo, ambalo amelitaja kuwa kiungo muhimu katika kuponya na kuunganisha taifa.
Kwa mfano, mwezi huu Dkt Ruto amedai kuwa chama cha ODM kinatumia pesa za umma kujipanga kwa siasa za 2022, kwa kisingizio cha kupigia debe BBI.
“Sisi tulikubaliana kuhusu yaliyomo kwenye BBI, tutafute nakala za kutosha wananchi wajisomee na wajifanyie uamuzi. Ni lini ilibadilika kwamba ile tulikubaliana imebadilika, sasa tunaambiwa kuna viongozi wa vyama ndio wanataka kusomea na kuamulia wananchi?
“Nani amepinga BBI, kama kila Mkenya amekubali maneno ya BBI, hii kampeni yote inafanywa ni ya nini? Ama ni ya kutafuta jinsi ya kufuja pesa za serikali,” Naibu Rais alisema.
Kinaya ni kuwa, Rais Kenyatta amekuwa akimsifu Bw Odinga na kusema binafsi, anakumbatia BBI.
Baadhi ya wafuasi wa Rais Kenyatta wametaja yanayomkumba Dkt Ruto kuwa mwiba wa kujidunga, wakisema amekuwa akimkosea Rais heshima.
“Amekuwa akimkaidi Rais kila wakati, Rais akisema tuache siasa ndiye anaongoza, huku ni kumkosea Rais heshima,” akasema aliyekuwa mwenyekiti wa Jubilee David Murathe, alipokuwa katika mahojiano na runinga ya K24.
Katika ishara kuwa mambo bado, kuna duru kuwa viongozi ambao wamehusishwa na ufisadi hawataruhusiwa kushiriki uchaguzi wa chama cha Jubilee, na kuwa Rais Kenyatta ataendelea kushikilia wadhifa wa kiongozi wa chama hicho.
Baadhi ya wafuasi wa Rais wamemlaumu Dkt Ruto kwa yanayomkumba, wakisema amekuwa akijaribu kung’aa kumshinda mkubwa wake.
“Tuna viongozi wengi duniani ambao wamekuwa manaibu rais, lakini huyu wetu amejifanya ni kama yeye ndiye mkuu, ni kama hakuna Rais. Kwa kuwa alipewa nusu ya serikali inamfanya kujiona kama amekuwa Rais,” mbunge maalum Maina Kamanda alisema mnamo Januari 13, katika kikao kilichomtaka Dkt Ruto kujiuzulu.