Aliyekuwa akijifanya brigedia wa KDF akamatwa
MWANAUME aliyekuwa akijifanya brigedia wa Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) na kudanganya watu kuwa angewapa ajira katika jeshi amekamatwa.
Katika taarifa iliyotolewa Jumanne, Novemba 18, Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) ilisema kuwa mshukiwa alikamatwa katika nyumba yake mtaani Kilimani, Nairobi akiwa amevalia sare kamili za Jeshi la Angani la Kenya.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mwanaume huyo alikuwa akidanganya vijana kwa kuwapa barua bandia za kujiunga na chuo cha mafunzo ya makurutu kilichoko Eldoret.
DCI ilisema kuwa katika msako huo, vitu kadhaa vilipatikana, vikiwemo nyaraka zilizokuwa na nembo ya Wizara ya Ulinzi, barua sita za kujiunga na jeshi zikiwa na nambari moja, fomu saba za alama za vidole, na vifaa vingine vinavyohusishwa na uhalifu.
“Maafisa wa DCI kutoka Parklands wamemkamata mshukiwa aliyekuwa akijitambulisha kama brigedia wa KDF, akitoa matumaini kwa raia wasio na hatia na kujipatia pesa kwa udanganyifu,” ilisema taarifa ya DCI.
“Mshukiwa huyo ambaye ‘alijipachika cheo’ kutoka raia hadi brigedia wa KDF bila hata kushuhudia gwaride, amekuwa akiwatapeli vijana kwa barua feki za kujiunga na chuo cha mafunzo ya makurutu wa jeshi Eldoret,” ikaongeza taarifa hiyo.
DCI iliwataka wananchi kuepuka njia za mkato katika ajira za sekta ya usalama, ikisisitiza kuwa uajiri halisi ni bure, wa haki na wenye uwazi.
Kukamatwa kwa mshukiwa kulijiri wiki tatu baada ya kukamilika kwa zoezi la uajiri wa KDF, lililoanza Jumatatu, Oktoba 13 hadi Jumamosi, Oktoba 25.
Kabla ya zoezi hilo, KDF ilisisitiza waombaji kufuata masharti ya maombi, ikiwemo kuwasilisha maombi kwa njia ya mtandaoni.
Mwananchi aliyestahili kujiunga alipaswa kuwa Mkenya mwenye kitambulisho cha kitaifa, PIN ya KRA na vyeti halisi.
Zoezi hilo lilifanyika kote nchini, likiongozwa na timu kutoka Jeshi la Nchi Kavu, Jeshi la Anga na Jeshi la Wanamaji katika vituo vilivyoteuliwa.