Habari

Aliyekuwa Mkuu wa Utumishi wa Umma aaga dunia

May 14th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

ALIYEKUWA Mkuu wa Utumishi wa Umma Jeremiah Kiereini amefariki Jumanne asubuhi jijini Nairobi akiwa na umri wa miaka 90.

Amefariki katika Nairobi Hospital alikokuwa amelazwa baada ya kuugua.

Kiereini ambaye alihudumu kwa muda mrefu katika utumishi wa umma alishikilia wadhifa huo katika miaka ya themanini (1980s) wakati wa enzi ya Rais Mstaafu Daniel Moi.

Baada ya kusfaafu alipiga mbizi katika ulimwengu wa biashara na katika miaka ya hivi karibuni alihudumu kama mwenyekiti wa kampuni ya magari ya Cooper Motor (CMC).

Marehemu Kiereini pia anahusishwa na kampuni zenye utajiri mkubwa zikiwa ni pamoja na ile ya kutengeneza pombe, East African Breweries Ltd, CFC Stanbic Holdings, Liberty Holdings, na Unga Group.

Mfanyabiashara huyo mkwasi amemuacha mjane, Emma Muringi Kiereini na watoto wanne. Bi Kiereini ndiye Mwafrika wa kwanza nchini Kenya kushikilia wadhifa wa Muuguzi Mkuu.

Marehemu ni shemejiye Mwenyekiti wa Kampuni ya Royal Media Services SK Macharia na Balozi Njeru Githae.

Rais Uhuru Kenyatta alikuwa wa kwanza kutuma salamu za pole kufuatia kifo cha Bw Kiereini akimtaja kama mtumishi wa umma aliyefanya kazi kwa “moyo wa kujitolea”.