Aliyetisha mashahidi ahukumiwa kifungo cha jela miaka 14
Na RICHARD MUNGUTI
MZEE aliyeshtakiwa kwa kutisha mashahidi katika kesi ya ulipuaji matatu kwa gruneti ambapo abiria watatu walifariki Mei 4, 2014, amehukumiwa kifungo cha miaka 14 gerezani bila faini.
Hata hivyo, mahakama imeamuru akae jela miaka 10 kwa sababu alikuwa kizuizizini kwa muda wa miaka minne.
Sar Guracha Haro alipatikana na hatia Ijumaa na Hakimu Mkuu wa Milimani, Nairobi, Bw Francis Andayi.
Bw Andayi amesema kuwa kosa alilofanya Guracha ni baya kwa sababu alivuruga haki katika kesi aliyoshtakiwa pamoja na mwanawe Warque Dejene Sar.
Hakimu amesema makosa aliyofanya yanaweza kufanya haki kutotendeka.
“Makosa aliyofanya mshtakiwa ya kuwatisha mashahidi ni mabaya kwa sababu wahalifu watazoea kutoadhibiwa katika makosa wanayofanya,” amesema Bw Andayi.
Alisema wahalifu watakuwa wanatenda makosa na kuenda nyumbani kuponda raha na kupumzika huku wakijua hakuna hata shahidi mmoja atafika mahakamani kueleza yaliyojiri.
Mahakama imesema kitendo hicho ni cha kuua sheria polepole ili isitumiwe kuwaadhibu wahalifu.
Katika kesi hiyo ya kulipua kwa gruneti matatu hiyo katika barabara kuu ya Thika Superhighway, Guracha na mwanawe Dejene waliachiliwa kwa kukosekana ushahidi.
Akiwaachilia Guracha na Dejene, hakimu alisema hakuna ushahidi uliowasilishwa kuthibitisha kwamba wawili hao waliunga mkono ugaidi licha ya mashahidi kusema wawili hao walipokea Sh85,000 kupitia M-Pesa kutoka kwa ajenti ajulikanaye Cool Breeze katika mji wa Kakuma.
Karibu na mpaka
Hakimu alishutumu upande wa mashtaka kwa kutegemea ushahidi kuwa Guracha alionekana akitembea katika mpaka wa Kenya na Somalia.
Bw Andayi amesema shahidi mkuu katika kesi hiyo alitishwa na hakurudi tena mahakamani.
“Mshtakiwa alifaulu katika azma yake ya kukwepa makali ya sheria kwa kutisha mashahidi,” akasema Bw Andayi.
Akaongeza: “Utatumikia miaka 10 ijapokuwa nimekufunga miaka 14. Miaka minne umekuwa rumande na hii korti inachukulia ulikuwa kizuizini.”