HabariSiasa

Asili ya Mzee Moi ni Mlima Kenya – Serikali

February 10th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na VALENTINE OBARA

ASILI ya Rais wa pili wa Kenya Daniel arap Moi ilikuwa ni Mlima Kenya kulingana na tovuti mpya ya serikali ya https://www.moi.go.ke iliyobuniwa na kuzinduliwa Jumatatu kumuenzi Mzee Moi.

“Moi alipewa jina la baba yake Kimoi arap Chebii, ambaye mababu zake walihamia Milima ya Tugen katika Kaunti ya Baringo karne ya 19 kutoka miteremko ya Mlima Kenya,” taarifa kwenye mtandao huo inaeleza.

Taarifa hiyo inasema kuwa mababu wa Mzee Moi walikuwa wamehama Mlima Kenya kuepuka mapigano ya mara kwa mara na Wamaasai

Kwa sasa jamii zinazopatikana katika miteremko ya Mlima Kenya ni Agikuyu wanaoishi kaunti za Nyeri na Kirinyaga na Ameru wanaoishi Kaunti ya Meru.

Wamaasai ambao huenda walikuwa wakipigana na mababu wa Mzee Moi wanapatikana katika Kaunti ya Laikipia ambayo pia iko karibu na Mlima Kenya.

Mzee Moi alizaliwa mnamo Septemba 2, 1924 katika kijiji cha Kurieng’wo, lokesheni ya Sacho, Kaunti ya Baringo.

Alichukua urais mnamo 1978 kufuatia kifo cha rais wa kwanza Mzee Jomo Kenyatta na akaongoza Kenya kwa miaka 24 hadi alipokabidhi madaraka kwa Mwai Kibaki mnamo 2002.